ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Baada
ya kuwaza kidogo alikumbuka kuwa bastola yake ilikuwa imebakiza risasi moja
ndani. Ndipo alipoamua kujimaliza na yeye kwa kujipiga risasi.
SASA ENDELEA.......
Wakati huo nilikuwa
namfuatilia kwani machale yangu yalikuwa yamenicheza. Wakati anaondoka nyumbani
alikuwa kashaniambia kuwa anaenda kwa mpenzi wake ila alikuwa akienda bila ya
taarifa huku akiyavunja masharti aliyokuwa amepewa na mpenzi wake huyo.
Niliamua kumfuatilia
ili nikashuhudie ‘timbwilitimbwili’ nililokuwa nikilitegemea kuibuka baada ya
kaka James kufika kwa mpenzi wake huyo. Hata kama yangetokea mapigano kisha
kaka yangu akazidiwa basi mimi ningekuwepo nyuma yake kuokoa jahazi.
Hata hivyo aliniacha
njiani kwani alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi mno. Mimi nilikuwa naogopa
ajali hivyo nikawa naendesha mwendo wa kistaarabu.
Kwenda kwangu
polepole ndiyo kulinifanya nimkose kaka James katika dunia hii kwani
nilichelewa kiduchu mno. Wakati naufikia mlango wa chumba walichokuwamo kina
Neila, tayari kaka James alikuwa kashakitekenya kitufe cha kufyatulia risasi
huku akiwa amejilenga kwenye kichwa chake.
Nilimshuhudia kaka
James akianguka mzima mzima kisha akakata roho. Ndipo nilipopoteza fahamu na
kushindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.
Fahamu zilinijia
masaa matano mara baada ya tukio hilo kutokea. Nilijikuta nipo wodini huku
nikiwa nimetundikiwa drip ya maji. Nilishangaa sana kujikuta nipo hospitali.
Katika kuvuta
kumbukumbu nilikumbuka jinsi mambo yalivyokuwa masaa matano yaliyokuwa
yamepita. Nilikumbuka kuwa kaka James hakuwepo tena duniani.
Nilizidi
kuchanganyikiwa, akili yangu ikazidi kuvurugika baada ya kukumbuka hilo tukio
lililokuwa na tanzia kubwa katika moyo wangu na akili yangu kwa ujumla.
Sikuona kabisa
mantiki ya kuendelea kubaki hospitali wakati nyumbani kulikuwa na msiba wa
marehemu kaka yangu. Sikujua ni vipi mipango ya mazishi ilikuwa inapangwa huko
kwani mimi ndiyo nilikuwa ndugu wa pekee wa marehemu. Kwa kifupi mhusika mkuu
wa msiba huo nilkuwa ni mimi.
Nilipojaribu kuangaza
angaza niliona karibu wagonjwa wote wamelala kwenye vitanda vyao kila mmoja.
Sikuona muuguzi wala dakitari yeyote aliyekuwemo kwenye wodi hiyo.
Bila kuchelewa wala
kuduwaa niliichomoa sindano ya drip na kutoka mbio kuelekea nyumbani kuungana
na majirani kuomboleza kifo cha kaka James.
Kwa vile James
alikuwa mtu mashuhuri sana katika mji huo, tayari taarifa za kifo chake
zilikuwa zimeshazagaa mtaani na katika mji wote kwa ujumla.
Nilipofika nyumbani
niliwakuta watu wengi wameshakusanyika. Hata hivyo mwili wa marehemu ulikuwa
upo hospitali umehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi. Nilijumuika na watu waliokuwa
wameshafika, maombolezo yakaendelea.
Watu walizidi
kumiminika kuja kunipa faraja kwenye msiba huo. James alikuwa ni mtu wa watu,
alijua kukaa vizuri na majirani pamoja na watu wengine aliokuwa akifahamiana
nao. Hali ya watu kujaa ilinifariji kwa kiasi fulani ingawaje moyo wangu
ulikuwa umeghubikwa na majonzi yasiyokuwa kifani.
******************************
ITAENDELEA....
No comments:
Post a Comment