ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Watu
walizidi kumiminika kuja kunipa faraja kwenye msiba huo. James alikuwa ni mtu
wa watu, alijua kukaa vizuri na majirani pamoja na watu wengine aliokuwa
akifahamiana nao. Hali ya watu kujaa ilinifariji kwa kiasi fulani ingawaje moyo
wangu ulikuwa umeghubikwa na majonzi yasiyokuwa kifani.
******************************
SASA ENDELEA.......
Pamoja na kwamba ni
miezi kadhaa ilikuwa imepita tangu kifo cha kaka James kutokea, akili yangu
ilikuwa haijachanganya kabisa. Kila nilichokuwa najaribu kukifanya nilikiona hakifai.
Kifo hicho kilikuwa
kimetonesha donda jingine kwenye mtima wangu ambalo lilikuwa bado halijapona.
Donda hilo nilikuwa nalifananisha na donda ndugu kwani lilikuwa limechukua muda
mrefu sana bila kupona ndani ya moyo wangu.
Usiombe kupata
majeraha palipo na donda ndugu mpenzi msomaji. Hebu fikiria maumivu yake
yatakavyokuwa. Ni zaidi ya uchungu!
Donda lililotoneshwa
na kifo cha kaka James ni lile lililokuwa limeachwa na kipenzi cha roho yangu
marehemu Anna pamoja na wazazi wangu, hasa hasa kile cha Anna.
Kuondoka kwa Anna
katika dunia hii kuliniathili pakubwa sana kisaikolojia na athari yake hiyo
ilikuwa bado haijaisha moyoni mwangu.
Mpaka leo huwa sipati
jibu ukiwa wanaoupata wale wanaoondokewa na wenzi wao wa ndoa wanaowapenda kwa
dhati. Ikiwa mimi niliipata freshi kwa mpenzi tu ambaye tulikuwa hata bado
hatujaoana, wao sasa inakuwaje ukizingatia tayari wameshaonja tamu ya ndoa?
Marehemu Anna alikuwa
ni msichana wa pekee ambaye nilitokea kumpenda kipindi nasoma. Mimi nilikuwa
nasoma elimu ya sekondari yeye alikuwa bado yupo shule ya msingi.
Uzuri wa sura yake,
umbo pamoja na tabia ndivyo vilikuwa vimenichengua mtoto wa kiumi mpaka nikawa
sijiwezi, nikafa na kuoza kwake kama vijana wa kileo wasemavyo. Mtoto alikuwa
yupo kamili gado, kamili kila idara.
Mpaka wa leo huwa
natafutia msichana mwenye sifa kama zake lakini naambulia hola! Wasichana wa
namna hiyo ni adimu sana kuwapata, yaani ni sawa na kumsaka bikira uswahilini
kwani unaweza ukakesha bila hata ya kumpata.
Mapenzi yetu hayakuwa
kama mapenzi yale yanayofanywa na vijana wa siku hizi, mapenzi ya kuanza kuzini
kabla hata hamjafunga ndoa. Eti wao husema huwezi ukauziwa mbuzi kwenye gunia;
wapi ndugu zangu hizo ni roho za pepo wachafu tu, pepo wa uzinzi.
Ndiyo zao vijana wa
siku hizi, hasa wavulana. Utakuta wanakwambia kumuoa mwanamke huku hujafanya
naye mapenzi ni kosa la jinai kwani unaweza ukakuta hayawezi ‘mahabati’,mwenye
kutulia kama gogo kwenye mambo fulani. Wanasema yote hayo ni tisa, kumi ukute
bwawa na siyo kisima, au ukutane na ile timu ya Songea; unaweza ukatangaza
taraka. Hiyo ndiyo mitazamo yao.
Mimi hayo sikujali
kwani niliona ni upuuzi na ulimbukeni mkubwa unaotokana na utumwa wa mapepo ya
uzinzi. Kutokana na misingi mizuri ya kidini niliyokuwa nimefundishwa tangu
utotoni niliamini kuwa hakuna linaloshindikana mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kama yeye huwatakasa
mpaka wenye ukoma, kwa nini asikibadilishe kitu chochote kinacholeta kikwazo
kwako kilichopo kwenye mwili wa mwenzi wako wa ndoa uliyemuoa kwa ndoa halali
kabisa? Yote yanawazekana.
Hivyo ndivyo mitazamo
wetu ilivyokuwa. Bahati nzuri ni kwamba Anna alikuwa bado hajaupoteza usichana
wake na mimi nilikuwa sijaupoteza uvulana wangu. Wote tulikuwa safi kabisa.
Pamoja na kupendana
kwetu lakini tulikubaliana kutofanya mapenzi mpaka tuje kufunge ndoa kwani
kinyume na hapo ni dhambi kwa Mungu, dhambi ya kuzini ambayo inawatafuna vijana
wengi wa siku hizi.
Huo ndiyo huitwa
upendo wa kweli, mapenzi yasiochuja mpaka uzeeni. Siyo mapenzi feki ambayo leo
mko pamoja halafu kesho mnazinguana na kushika hamsini zake kila mmoja.
Kifo cha Anna ndiyo
kilizima taa za upendo moyoni mwangu na kuacha giza totoro ambalo mpaka leo ni
athari kubwa kwangu.
Alikuwa anajipenda,
alikuwa anajiheshimu, wala hakuwa mapepe na ndio maana vijana wengi wa mtaani
walitamani sana awe wao matokeo yake waliishia kula ‘vibuti’ vya uso.
Amini usiamini siku
zote mti wenye matunda ndiyo hupigwa mawe. Kutokana na usemi huo, kipenzi Anna
nilimfananisha na mti wa mnazi ambao hata ukiupopoa kwa mawe huwezi kuangusha
nazi wala dafu. Kumbe nilikuwa najidanganya kwani kuna wakwezi ambao hupanda
mpaka matunda yaliko kisha huanza kuyasanifu kwa vyovyote vile wanavyotaka.
Hicho ndicho
kilichotokea kwa marehemu Anna. Pamoja na kuwa na msimamo zaidi ya binti wa
kilokole, ilifika siku maagano yetu yakavunjika japokuwa siyo kwa ridhaa na
utashi wake.
Ilikuwa ni siku ngumu
sana kwake; siku aliyorubuniwa na dada yake kisha wakaenda kwenye sherehe ya
kuzaliwa ya mpenzi wa huyo dada yake. Kumbe kulikuwa na mipango kabambe ya
kumwingiza kipenzi changu kwenye jaribu zito lililokuja kupelekea kifo chake.
ITAENDELEA.....
No comments:
Post a Comment