Wednesday, November 6, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 40

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Kumbe kulikuwa na mipango kabambe ya kumwingiza kipenzi changu kwenye jaribu zito lililokuja kupelekea kifo chake.
SASA ENDELEA.......

Kuna kijana mmoja ambaye alikuwa akimtaka Anna kimapenzi siku nyingi lakini ikashindikana. Kwenye hicho kisherehe naye alikuwepo.
Baada ya kumuona Anna kijana kijana huyo akasema kuwa lazima lengo lake litimie, ndipo alipomchanganyia dawa za kulewesha kwenye soda na hatimaye akalewa na akawa hajielewi.
Baada ya kufanya hivyo kijana huyo alijichukulia mzigo kiulaini na kwenda kuutumia jinsi alivyotaka. Lengo lake lilikuwa ni kufanya mapenzi na Anna, kweli alifanikiwa japokuwa Anna alikuwa hajitambui.
Tukio hilo lilimuumiza sana kipenzi changu. Hata hivyo wakati huo mimi nilikuwa masomoni hivyo hakuweza hata kupata faraja kutoka kwangu. Miezi miwili baadaye tulifunga shule. Ndipo niliporudi nyumbani na kukuta habari za kubakwa kwa Anna ambazo ziliurarua moyo wangu.
Tunu ya usichana wa Anna ambayo alikuwa ameitunza kwa ajali yangu ilikuwa tayari imeshahujumiwa. Hakuwa bikira tena. Iliniuma sana kusikia hivyo. Hata hivyo sikutaka kuukatisha uhusiano wetu kwa sababu ya hilo, nilimwambia kuwa tutakuwa pamoja licha ya kwamba tunu yangu ilikuwa imeshahujumiwa.
Ndipo nilipomshauri aende kuangalia afya yake huenda siku hiyo alipata maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Naye bila ubishi alienda, hata hivyo majibu yalikuwa safi.
Siku kadhaa zilipita. Nikiwa sijui hili wala lile nilipokea taarifa za kifo cha Anna, taarifa ambazo zilizidi kuuchoma moyo wangu.
Taarifa hizo zilisema kwamba Anna alikuwa amekufa baada ya kufanya jaribio la kutoa mimba. Niliposikia hivyo nilijua moja kwa moja mimba hiyo iliingia siku ile alipobakwa na yule kijana.
Ndipo nilipozidi kuumia na kujihisi mpweke zaidi ya kinda lililoachwa na mama likabaki peke yake kwenye kiota. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha ya Anna kwa hapa duniani ingawa mpaka leo moyoni mwangu yu hai.
Tukio hilo liliniacha na kidonda kikubwa sana ndani ya moyo wangu. Mpaka nakuja kuondokewa na kaka yangu kidonda hicho kilikuwa hakijapata hata dalili za kupona, kikawa kimegongomewa msumari mwingine tena mkubwa zaidi.
Aliyekuwa mstari wa mbele kunifariji juu ya machungu ya kuondokewa na Anna naye alinitoka, tena kwa kifo cha ghafla ghafla huku nikimshuhudia wakati roho inaachana na mwili wake. Hakika lilikuwa ni pigo mjaarabu.
Huku nikiwa na majonzi yangu tele moyoni niliendelea kulisongesha huku nikipata faraja kutoka kwa majirani na rafiki zangu wa karibu, faraja ambayo hata haikukidhi mahitaji ya upweke uliokuwepo ndani ya moyo wangu.
Kitu kingine ambacho kilianza kuniacha hoi ni hizo mali zilizokuwa zimeachwa na kaka James. Nilizidi kuchanganyikiwa kwa jinsi zilivyokuwa zikipukutika na kuisha bila kuelewa zinaishaje.
Biashara zote zikawa haziendi. Nikienda kwenye maduka mauzo yalikuwa mabovu, kampuni ya usafirishaji nayo ikazidi kufilisika siku hadi siku. Ajali za mara kwa mara zikawa zinatokea kwenye malori ya kusafirisha mizigo kwanye kampuni hiyo. Nilizidi kuchoka.      
Baada ya kuona mambo yanazidi kwenda kombo niliamua kuanza kupiga bei mali moja baada ya nyingine. Nilianzia kuuza nyumba aliyokuwa kahongwa Neila, mwanamke aliyepigwa risasi na kaka James.
Mara baada ya kuiuza nyumba hiyo, niliyatangazia dau magari mawili ya kifahari yaliyokuwa yameachwa na kaka James. Gari moja ni lile alilohongwa Neila; mwanamke aliyekuwa akijidai ana mapenzi ya kweli kwa kaka James kumbe hamna chochote. Mwanamke ambaye alisababisha kifo cha kaka yangu huyo.
Gari la pili ni lile alilokuwa akitumia kaka James. Yote yalikuwa ni magari ya kifahari. Nilibakiza gari moja ambalo nilikuwa nalitumia mimi. Hilo sikutaka kuliuza.
Ndani ya miezi sita nilikuwa nimeshauza kila kitu; maduka, nyumba pamoja na kampuni ya usafirishaji. Lengo langu lilikuwa ni kuhama kabisa mji huo.
  Nilipomaliza michakato yote nilihama mji huo na kuhamia mji mwingine ambako nilienda kununua nyumba na kuendelea na maisha kama kawaida. Nilianza kufanya biashara zangu huko.
Nyumba hiyo ilikuwa kubwa mno kukaa peke yangu kwani nilikuwa bado nahisi upweke kutokana na kuondokewa na nguzo yangu muhimu katika dunia hii.
Ndipo nilipoamua kukipangisha chumba kimoja na mpangaji aliyekuja kupanga alikuwa ni marehemu Kishoka. Alikuwa ni kijana mstaarabu sana ambaye hakuwa na makuu.
Maisha yetu yalizidi kuwa ya furaha kadri siku zilivyozidi kusonga. Tukawa tunaishi kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu kila mmoja akiwa na meno thelethini na mbili.
Kiumri tulikuwa hatupishani sana japokuwa alikuwa ananizidi miaka mitatu. Nilipomuita kaka naye aliniita kaka. Pamoja na kunizidi umri lakini na mimi nilikuwa mwenye nyumba wake.
Ilifikia wakati nikamwambia asiwe ananilipa kodi ya nyumba kwani urafiki wetu ulikuwa umefikia hatua nyingine. Akawa anaishi bila kulipa kodi ya pango siku zote.
Mpaka matatizo ya kifo chake yanatokea tulikuwa tunaishi naye kama ndugu, kifo ambacho kilikuja kikanigharimu hukumu ya kunyongwa nikisingiziwa kuwa mimi ndiye niliyemchinja.
Nilizidi kuchanganyikiwa kwa kuona maisha yangu yakiandamwa na mikasa, mikosi na ndege mbaya kila wakati. Kichwa kilizidi kuuma.

                        ********************
ITAENDELEA.....


No comments:

Post a Comment