Mlevi mmoja aliingia kwenye daladala na kukaa siti ya mbele halafu akaweka begi lake kwenye siti ya pembeni kisha akapitiwa na usingizi.
Mara akaingia mlevi mwingine kwenye daladala hiyo na kulitoa begi la mlevi wa kwanza kisha akakaa.
Mlevi wa kwanza alipoamka alipeleka mikono yake alipokuwa ameliweka begi na kuanza kufungua zipi ya suruali ya mlevi wa pili akidhania ya kwamba ni zipu ya begi lake, baada ya kufungua zipu alianza kupapasa ndani ya zipu hiyo. Kwa hasira akauliza,
"nani kaweka ndizi na machungwa kwenye begi langu?"
Unajua kilichotokea hapo ni kipi? Like hapo chini kisha nitakutumia jibu kwenye inbox.
Friday, December 27, 2013
Monday, December 23, 2013
MIRATHI YA KAKA KUANZA UPYA KWENYE PAGE YA Hakuna kulala, Mpaka kieleweke?
Hakuna kulala, Mpaka kieleweke?
kama hukubahatika kusoma matoleo ya mwanzo ya hadithi ya "MIRATHI YA KAKA" ama unataka kukumbushia utamu uliomo kwenye hadithi hiyo tamu na yenye kusisimua, bofya kwenye link hiyo hapo juu kisha uilike, utapata post za hadithi ya mirathi ya kaka kuanzia matoleo ya wanzo. pia usisahau ku-like na kutupia comment zako bada ya kumaliza kusoma! .
Wednesday, December 18, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 56
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa
gerezani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa
kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na
kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo
zoezi. Sasa Brighton tayari yupo uraiani na anachukuliwa na Sharifa na
kupelekwa kwenye hoteli na kuanza kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake
(yaani James) ulivyopatikana.......endelea
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Mara baada ya
kuongea hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na
kufumbua alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa
sana.
**************************
SASA ENDELEA..........
Asubuhi ilifika,
ilikuwa ni asubuhi ya kwanza kuiona nikiwa uraiani baada ya kukaa rumande na
hatimaye gerezani kwa miaka mingi. Niliamkia kwenye hoteli hiyo hiyo niliyokuwa
nimepelekwa na Sharifa jana yake.
Mara baada ya kuamka
nilitupia jicho langu kitandani kuiangalia brificase iliyokuwa imejaa mapesa
niliyokuwa nimeachiwa na Sharifa. Niliiona imetulia. Nikajiinua kisha
nikaifungua na kuiona minoti imejaa tele.
Nilipoangalia mezani
niliziona funguo za gari niliyokuwa nimeachiwa. Kwa bahati nzuri chumba
nilichokuwa kilikuwa kipo upande tuliokuwa tumeegesha gari. Nikaamua
kuchungulia nje ili kujiridhisha kama gari hilo lilikuwepo kweli. Nikaliona
limetulia.
Wazo nililokuwa nalo
usiku wakati Sharifa hajaondoka ni kukataa katakata kufuata masharti yote
niliyokuwa nikishinikizwa kuyafanya; masharti ya kuoa mwanamke kisha
akishanizalia mtoto nimtoe kafara pamoja na mtoto aliyemzaa, na baada ya hapo
niwe natoa kafara mtu mmoja kila mwaka ambaye ni mfanyakazi wangu ama mteja
wangu wa aina yoyote ile.
Hata hivyo baada ya
Sharifa kunishika kichwani muda mfupi kabla ya kuyeyuka ghafla wazo hilo nalo
liliyeyuka kabisa kichwani mwangu. Nikaanza kujiona kama mtu anayechezea
shilingi kwenye tundu la msala.
Nililipima jambo hilo
usiku kucha kwa mapana na marefu, nikaona hakuna sababu yoyote ya kulipiga teke
debe la bahati kama hilo. Kitu kilichonipa moyo ni kwamba sikutakiwa kumtoa
kafara ndugu yangu yeyote wa karibu zaidi ya mke ambaye nitamuoa kwa ajili hiyo
pamoja mtoto nitakayemzaa kwa ajili hiyo.
Nikaona ni bora
nikubaliane na shinikizo la Sharifa ili nitengeneze maisha yangu, niwe mmoja
kati ya matajiri wakubwa nchini na duniani pia. Moyo wangu uliridhia kabisa
kutajirika kwa njia hiyo, njia ya nguvu za giza na ya kishetani huku nikiwa
tayari kuendelea kuteketeza watu kila mwaka kwa kuwatoa kafara ili nizidi
kuulinda utajiri wangu huo.
Pesa nilizokuwa
nimeachiwa na Sharifa zilizidi kunipa jeuri, jeuri ya kwenda kununua nyumba
sehemu yoyote katika nchi hiyo. Jambo la kuendelea kuishi kwenye mji huo sikuwa
nalo kabisa akilini mwangu, hivyo nikaamua kuondoka asubuhi hiyo kwenda mji
mwingine uliokuwa mbali na mji huo.
Niliinuka na kwenda
maliwatoni kujimwagia maji mwilini mwangu. Nilipotoka nilivaa nguo zangu kisha
nikainua simu ya mezani iliyokuwemo hotelini humo kuangiza kifungua kinywa.
Haukupia muda sana
mlango ukagongwa, nami nilifungua na kumuona dada aliyekuwa amebeba trei
(chano) iliyokuwa imesheheni mazagazaga kwa ajili ya kifungua kinywa.
Kabla hajaondoka
nilichukua noti moja iliyokuwa na rangi ya kaki na kumpa ikiwa ni malipo ya
kifungua kinywa hicho.
“Haina haja ya kulipa maana kila kitu
kimelipiwa.” Aliniambia mwanadada huyo.
Hata hivyo ili
kumuonyesha kuwa nilikuwa ni bilionea mtarajiwa kwa wakati huo, nilimwambia
achukue tu hiyo pesa kwani nilikuwa nimeshaitoa kwenye mahesabu. Naye bila kuvunga
aliipokea, si alikuwa kapewa!
“Samahani dada yangu
kama nitakukwaza, ningependa kulijua jina lako.” Nilijikuta namchombeza zikiwa
ni harakati za kutaka kutangaza nia katika suala zima la mapenzi.
Bila kinyongo wala
malingo msichana huyo alinionyesha jina lake kwenye kitambulisho chake cha kazi
alichokuwa amekining’iniza shingoni.
Nililisoma jina na
kujikuta naachia tabasamu.
“Kumbe unaitwa Anna, jina lako lina historia
ndefu sana katika maisha yangu.”
“Historia gani tena kaka yangu?”
“Kwanza mama yangu mzazi alikuwa akiitwa jina
hilo, pili kuna msichana ambaye nilitokea kumpenda kupita kiasi naye alikuwa
akiitwa Anna, ni jina muhimu sana katika maisha yangu.”
“Kumbe! Basi na mimi naitwa hivyo!”
“Natabiri na wewe utakuwa na historia ndefu
sana katika maisha yangu,”
“Yaweza kuwa!” Aliongea Anna na kuanza kunipa
mgongo ili aondoke.
Bila kufikiri wala
kuwaza nilijikuta naropoka kumuomba namba ya simu ama mawasiliano yoyote. Pale
pale alinitolea kadi yake ya biashara (business card) iliyokuwa na kila aina ya
mawasiliano aliyokuwa akitumia.
“Asante sana mrembo!”
“Usijali!” Alimalizia maneno hayo huku
akifungua mlango na kuondoka zake.
Taratiibu kabisa
nilijongea kwenye kimeza kilipokuwepo chano cha mapochopocho ya chakula cha
asubuhi. Pasipo kuvunga nilikaa na kuanza kujichana kwa raha zangu. Kilikuwa ni
kifungua kinywa cha haja, waswahili wa siku hizi wanakwambia ‘msosi
draft’ulioenda shule.
Muda mfupi baada ya
kumaliza kushambulia kifungua kinywa niliondoka kwa mwendo wa madaha mpaka
kwenye mchuma wangu huku nikiwa nimening’iniza kibrificase changu mithili ya
kibosile ama fisadi aliyefutuka tumbo kwa kuchakachua fedha za umma.
Mpaka nafika nje
sikumuona Anna, nilitamani sana japo tupungiane mkono wa kuagana ili
nimringishie gari langu la kifahari, lakini haikuwezekana. Nadhani alikuwa
kwenye majukumu yake mengine hotelini hapo.
JE, BRIGHTON ATAMUONA TENA ANNA? NA
KAMA ATAMUONA ATAMWAMBIA NINI? FUATILIA TOLEO LIJALO!
Sunday, December 15, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 55
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa
gerezani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa
kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na
kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo
zoezi. Sasa Brighton tayari yupo uraiani na anachukuliwa na Sharifa na
kupelekwa kwenye hoteli na kuanza kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake
(yaani James) ulivyopatikana.......endelea
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Wakati nikiwa katika lindi la
mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.
SASA ENDELEA..........
“Usiwaze sana kwani kazi nzito ilishafanywa na
kaka yako, unachotakiwa wewe ni kuikamilisha tu na utakuwa bilionea wa
kuogopeka.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
“Daraja la kwanza
utakuwa umeshalivuka kwani wazazi wa James ni wazazi wako, pia kufa kwake
kutachukua nafasi ya ndugu wa karibu, kafara ambayo ilikuwa utolewe wewe.
Kitakachohitajika kwako ni kuoa mke kisha mkishazaa mtoto unamtoa kafara
akifuatiwa na mama yake, hapo utakuwa tayari umeshakamilisha daraja la pili.”
Alipozi kidogo.
Wakati wote huo
nilikuwa nimemsikiliza kwa makini. Baada ya kupozi kidogo aliendelea kuniambia
kuwa nikishaimaliza daraja la pili lile lililokuwa linafuata ni mteremko.
Daraja hilo ambalo ni daraja la tatu lilikuwa ni kumtoa kafara mtu mmoja kila
mwaka, mtu huyo anaweza kuwa ni mfanya kazi wako ama ni mteja wako. Hiyo hatua
ndiyo ilikuwa ni nyepesi kuliko zote kwani pale unamtoa mtu ambaye siyo ndugu
wa karibu.
Hata hivyo bado
ulikuwa ni mzigo mzito moyoni mwangu. Dhambi ya kuua nilikuwa naichukia na
nilikuwa sitegemei kabisa kuitenda katika maisha yangu.
Nilivuta kumbukumbu
ya maneno ya marehemu kipenzi changu Anna aliyoniambia kwenye ile ndoto niliyoota,
ndoto ya kutisha. Katika maneno yake alinisisitiza sana nisiue wala kujiua
kwani adhabu yake huwa ni kubwa mno.
Alinisisitiza nizidi
kutenda mema huku nikiongeza upendo kwa watu wote wanaonizunguka ili siku zangu
zikiisha duniani nikapumzike kwa amani na siyo kwa mateso.
Sasa mwanamke
aliyekuwa mbele yangu alikuwa ananishawishi nianze kuua kwa ajili ya kupata
utajiri, tena siyo kuua mara moja bali ni kuua kila mwaka mpaka pale maisha
yangu yatakapofika kikomo duniani. Niliogopa sana.
Kibaya zaidi jambo
lilikuwa limekaa kwenye njia panda, kama nisingefanya hivyo basi ningeuliwa
mimi. Kweli maisha ni matamu sana mithili ya asali mwitu japokuwa ni mafupi
zaidi ya watu wa Uturuki.
Hapo ndipo nilizidi
kuumiza kichwa. Lakini kumbukumbu ya maneno ya marehemu Anna ilionekana kunipa
nguvu. Nikajisemea kimoyomoyo kuwa ni bora nife kuliko kubeba dhambi mbaya na
nzito kama hiyo, dhambi ya kuua.
Nikiwa katika kuwaza
wazo lilinijia, nikaliona linafaa kulifanyia kazi. Nikataka kufumbua kinywa
changu ili nieleze msimamo wangu juu ya jambo lililokuwa lipo mbele yangu.
Kabla sijaongea chochote nilimuona Sharifa akisimama na kuniwekea mkono wake
kichwani. Mwili wote ulisisimka, nikajihisi kama nimepigwa shoti ya umeme.
Alipotoa mkono wake
juu ya kichwa changu aliniambia gari tuliyokuwa tumeenda nayo hotelini hapo
imekuwa yangu kuanzia wakati huo. Pia akaniambia pesa zote zilizokuwemo kwenye
brificase iliyokuwa mezani zote ni zangu.
Mara baada ya kuongea
hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua
alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.
**************************
ITAENDELEA..........
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 55
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa
gerezani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa
kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na
kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo
zoezi. Sasa Brighton tayari yupo uraiani na anachukuliwa na Sharifa na
kupelekwa kwenye hoteli na kuanza kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake
(yaani James) ulivyopatikana.......endelea
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Wakati nikiwa katika lindi la
mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.
SASA ENDELEA..........
“Usiwaze sana kwani kazi nzito ilishafanywa na
kaka yako, unachotakiwa wewe ni kuikamilisha tu na utakuwa bilionea wa
kuogopeka.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
“Daraja la kwanza
utakuwa umeshalivuka kwani wazazi wa James ni wazazi wako, pia kufa kwake
kutachukua nafasi ya ndugu wa karibu, kafara ambayo ilikuwa utolewe wewe.
Kitakachohitajika kwako ni kuoa mke kisha mkishazaa mtoto unamtoa kafara
akifuatiwa na mama yake, hapo utakuwa tayari umeshakamilisha daraja la pili.”
Alipozi kidogo.
Wakati wote huo
nilikuwa nimemsikiliza kwa makini. Baada ya kupozi kidogo aliendelea kuniambia
kuwa nikishaimaliza daraja la pili lile lililokuwa linafuata ni mteremko.
Daraja hilo ambalo ni daraja la tatu lilikuwa ni kumtoa kafara mtu mmoja kila
mwaka, mtu huyo anaweza kuwa ni mfanya kazi wako ama ni mteja wako. Hiyo hatua
ndiyo ilikuwa ni nyepesi kuliko zote kwani pale unamtoa mtu ambaye siyo ndugu
wa karibu.
Hata hivyo bado
ulikuwa ni mzigo mzito moyoni mwangu. Dhambi ya kuua nilikuwa naichukia na
nilikuwa sitegemei kabisa kuitenda katika maisha yangu.
Nilivuta kumbukumbu
ya maneno ya marehemu kipenzi changu Anna aliyoniambia kwenye ile ndoto niliyoota,
ndoto ya kutisha. Katika maneno yake alinisisitiza sana nisiue wala kujiua
kwani adhabu yake huwa ni kubwa mno.
Alinisisitiza nizidi
kutenda mema huku nikiongeza upendo kwa watu wote wanaonizunguka ili siku zangu
zikiisha duniani nikapumzike kwa amani na siyo kwa mateso.
Sasa mwanamke
aliyekuwa mbele yangu alikuwa ananishawishi nianze kuua kwa ajili ya kupata
utajiri, tena siyo kuua mara moja bali ni kuua kila mwaka mpaka pale maisha
yangu yatakapofika kikomo duniani. Niliogopa sana.
Kibaya zaidi jambo
lilikuwa limekaa kwenye njia panda, kama nisingefanya hivyo basi ningeuliwa
mimi. Kweli maisha ni matamu sana mithili ya asali mwitu japokuwa ni mafupi
zaidi ya watu wa Uturuki.
Hapo ndipo nilizidi
kuumiza kichwa. Lakini kumbukumbu ya maneno ya marehemu Anna ilionekana kunipa
nguvu. Nikajisemea kimoyomoyo kuwa ni bora nife kuliko kubeba dhambi mbaya na
nzito kama hiyo, dhambi ya kuua.
Nikiwa katika kuwaza
wazo lilinijia, nikaliona linafaa kulifanyia kazi. Nikataka kufumbua kinywa
changu ili nieleze msimamo wangu juu ya jambo lililokuwa lipo mbele yangu.
Kabla sijaongea chochote nilimuona Sharifa akisimama na kuniwekea mkono wake
kichwani. Mwili wote ulisisimka, nikajihisi kama nimepigwa shoti ya umeme.
Alipotoa mkono wake
juu ya kichwa changu aliniambia gari tuliyokuwa tumeenda nayo hotelini hapo
imekuwa yangu kuanzia wakati huo. Pia akaniambia pesa zote zilizokuwemo kwenye
brificase iliyokuwa mezani zote ni zangu.
Mara baada ya kuongea
hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua
alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.
**************************
ITAENDELEA..........
Thursday, December 12, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 54
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata
hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa
kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani na anachukuliwa na Sharifa na kupelekwa kwenye hoteli na kuanza
kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake (yaani James) ulivyopatikana.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Hayo
ndiyo mambo yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa
ya kaka yangu kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha
yake na ya wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila
Sharifa ndiye aliyekuja kuning’amua.
SASA ENDELEA..........
Pamoja na maelezo
hayo kuhusu kifo cha kaka James nilikuwa bado na maswali mengi sana kichwani
mwangu. Maswali menyewe ni pamoja na yeye Sharifa anahusika vipi na kafara hiyo
ama ana uhusiano upi na mganga wa kaka James?
Pia swali jingine
lililokuwa limetanda kwenye ubongo wangu ni kwamba mimi kosa langu lilikuwa ni
lipi hapo wakati aliyefanya maagano na mganga ni kaka yangu tu? Sikuwa na
majibu yake ila niliamini kuwa maswali hayo yangejibika kwa Sharifa.
Sikusita kumuuliza
kwani mpaka wakati huo nilikuwa nimemzoea na kumuona kama alikuwa ni mtu wa
kawaida wakati alikuwa si wa kawaida.
Nilianza na kutaka
kujua hao wataalamu hasa ni kina nani na wanapatikana wapi? Swali lilijibiwa.
Nikaambiwa kuwa wataalamu ni wale viumbe waliokuwa wamemuweka mganga huyo ili
aweze kufanya mawasilo nao katika kumpatia mtu utajiri aombapo. Sikutaka
kuendelea tena kudodosa juu ya swali hilo kwani tayari niling’amua kuwa
wataalamu hao ni majini ama pepo wachafu.
Nikahamia kwenye
swali la pili ambalo ni kutaka kujua Sharifa anahusikanaje na huyo mganga.
Alichonijibu wala sikukitila shaka, nikaachana na swali hilo mara baada ya
kupewa jibu.
“Na wewe una shirika
gani na yule mganga?”
“Ni mmoja kati ya wataalamu wake. Na mimi
ndiye nilichaguliwa kuhakikisha James anaaga dunia pamoja na kukuandama wewe
ili tukutie adabu, na ukiwa mgumu wa kuelewa utamfuata kaka yako aliko.”
Sikutaka
hata kuendelea kudodosa kwani majibu yenyewe yalikuwa yanajitosheleza. Tangu
mwanzo wa kuniandama mpaka kunitoa jela nilikuwa nimeshabaini kuwa Sharifa
hakuwa kiumbe wa kawaida. Alikuwa ni jini.
Hofu
ilizidi kujengeka alipotamka kauli ya kwamba hata mimi nikileta za kuleta
atanitia adabu ya kumfuata kaka James alikokuwa. Tafsiri ya maneno hayo ilikuwa
ni kwamba ataniua kwani James hakuwa Marekani wala Dubai bali alikuwa kuzimu.
“Kosa
langu hapo mimi ni lipi mpaka uniandame hivi?”
“Mirathi ya kaka yako.” Alijibu kwa mkato
kisha akafunga bakuli lake, yaani namanisha akanyamaza kimya.
Bado
kichwa changu kilikuwa na maswali ya kumhoji Sharifa. Mirathi ya kaka ilikuwa
imefanya nini? Nilizidi kuwaza kabla sijalitupia swali hilo kwa Sharifa.
Nilipomuuliza
alinijibu kuwa mali ya aina hiyo huwa haitakiwi kurithiwa na mtu yeyote yule.
Nilifanya kosa kubwa sana kurithi mali alizokuwa ameziacha kaka James wakati
zilikuwa ni za maagano.
Mpaka
hapo niliweza kuelewa kiini cha matatizo yangu. Nilijikuta nikianza kujuta
kurithi hizo mali pamoja na kuzaliwa pia. Niliweza kubashiri hatari iliyokuwa
inaninyemelea mbele yangu huku chanzo chote kikiwa ni mirathi ya kaka James.
“Kumbe
chanzo cha misukosuko yote hii ni hicho, sasa utanisaidiaje ili nijinasue
kwenye hili balaa?” Niliamua kumuuliza hivyo ili nijue hatima yangu.
“Dawa ya hapo ni moja tu”
“Ipi hiyo?”
“Kufanya yale yote tunayokutaka uyafanye,
zaidi ya hapo anza kujihesabu kuwa ni marehemu mtarajiwa.”
Hakuna
anayependa kufa jamani. Sikujua nifanye nini ili kujinasua kwenye urimbo
niliokuwa nimenasa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani. Sasa
nilizidi kuwa katika wakati mgumu.
Maelezo
ya mwanadada huyo hayakuwa na chembe ya utani ndani yake hata kidogo.
Alichokuwa anakisema alikuwa anakimaanisha. Uwezo wa kufanya hivyo alikuwa nao.
Tulibaki
tukiwa tumetumbuliana macho, mimi nikiwaza yangu kutokana na uzito wa jambo
ulivyokuwa. Nilikuwa najiona dhahiri ninavyodumbukia kwenye shimo lenye kina
kirefu nisiloweza kutoka tena.
Wakati
nikiwa katika lindi la mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa
kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.
“JE, SHARIFA ATAMWAMBIA NINI BRIGHTON? Tukutane
kwenye toleo lijalo.
Monday, December 9, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 53
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata
hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa
kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Masharti
hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia
kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika
ajali ya kutisha.
SASA ENDELEA..........
Habari
hii ndiyo iliyonitonesha majeraha yaliyokuwa yamejengeka ndani ya moyo wangu
mithili ya donda ndugu. Kuanzia hapo nilianza kumchukia James na kumuona ni
shetani mkubwa ambaye alikuwa anastahili kutupwa kwenye moto wa jehanamu.
Nilijikuta
nahukumu wakati maandiko ya Mungu yanatuambia tusikuhumu ili na sisi tusije
tukahukumiwa. Niliumia sana nilipoambiwa hiyo habari.
‘Ndiyo
maana mambo ya kaka James yalianza kuwa safi mara baada ya vifo vya wazazi
wetu.’ Niliwaza.
Wakati
huo huo nikakumbuka swali, nikaona nimuulize huyo huyo Sharifa kwani hata yeye
alikuwa ni mdau wa kafara hizo.
“Umesema kafara ya daraja la kwanza inahusisha
wazazi wote wawili na ndugu mmoja wa damu, mbona sasa baba yangu alikufa wakati
hakuwa baba wa kumzaa James?”
“Kwa kuwa alikuwa kamuoa mama mzazi wa James
na pia alikuwa na mapenzi ya baba kwake, basi kafara yake ilifana.” Alijibu
Sharifa.
Akaendelea
kunieleza kosa la James lilikuja kutokea baada ya kutakiwa kutoa kafara
nyingine ili kukamilisha kafara za kwenye daraja la kwanza. Hapo alitakiwa
ndugu yake wa karibu; mdogo mtu, kaka mtu, shangazi ama mjomba.
Kwa bahati mbaya sana
ndugu wa damu aliyekuwa yu ngali hai nilikuwa ni mimi peke yangu. Aliamua
kukaidi kunitoa kafara kutokana na mambo mawili.
Jambo la kwanza ni
upendo uliokuwepo baina yangu na yeye. Kusema kweli kaka James alikuwa
ananipenda kupita kiasi, na ndiyo maana hakuwa tayari kunitoa kafara.
Jambo lingine
lililomsababisha kaka James agome kunitoa kafara ni kwamba hapakuwa na ndungu
mwingine wa karibu zaidi yangu mimi. Kama angenitoa kafara basi angebaki bila
ndugu wa karibu katika dunia hii. Sasa kubaki bila ndugu wa karibu lilikuwa ni
jambo gumu sana kwake.
Nadhani hata wewe
mpenzi msomaji usingepata fursa ya kusimuliwa simulizi hii nzuri iliyojaa
vitisho vya lejaleja na yenye kusisimua kwani ningekuwa tayari nimeshalala
mauti.
Baada ya kuona
kunitoa kafara haiwezekani, James aliacha kabisa kwenda kwa mganga aliyekuwa
amemfanyia dawa ya kumpa utajiri huo wakati alitakiwa awe anaenda mara moja kwa
mwezi kufanya ibada. Muda wa kukamilisha kafara ya daraja la kwanza ulipita
huku akiwa hajakamilisha, akaongezwa muda wa ziada nao ukawa umepita.
Mganga alipoona James
kapuuzia agano hilo aliamua kumripoti kwa wataalamu wake ambao ndiyo waliokuwa
wanamwezesha kufanya uganga huo.
Wataalamu hao
walikasirishwa sana na kitendo chake cha
kujifanya mjanja na mwenye akili kuzidi wao waliokuwa wamempa maagizo yale.
Ndipo walipoamua kumtoa duniani kwa staili ya kujiua mwenyewe ili akaonekane
ana dhambi hata mbele za mwenyezi Mungu.
Japo kabla ya kutoa
adhabu hiyo walitoa muda wa kutosha kwake wakitegemea labda angejirudi na
kukamilisha agano lao, siku zilizidi kwenda bila ya mabadiliko yoyote ya kutaka
kujirudi kwa James.
Tena alipoona kakaa
muda mrefu bila kupatwa na matatizo yoyote ilhali alikuwa hajakamilisha kutoa
kafara alijua kuwa huenda zile zote zilikuwa ni danganya toto tu na vitisho
visivyokuwa na misingi yoyote. Baada ya muda wa nyongeza kuisha uhai wa James
ukawa ni halali ya wataalamu hao.
Hayo ndiyo mambo
yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa ya kaka yangu
kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha yake na ya
wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila Sharifa ndiye
aliyekuja kuning’amua.
NINI KITAFUATIA? USIKOSE TOLEO
LIJALO!!!
Friday, December 6, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 52
Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo
mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna
masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
“Tuendelee!”
niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu,
hivyo kama unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali
nitakayokuambia.” Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua
brificase iliyokuwa mezani.
SASA ENDELEA..........
Aliifungua
brificase na kuniambia niangalie. Naam! Ilikuwa imesheheni fedha za kigeni,
fedha ambazo zilikuwa zimebanwa katika maburungutu. Nilijikuta nikimeza mate
baada ya kuviona vitita hivyo.
“Kama
utakubaliana na ninachoenda kusema basi matumizi yako kwa siku yatakuwa ya pesa
kama hizi.” Mwanadada huyo alizidi kunitamanisha japokuwa nilikuwa sijajua
atakachokitaka kutoka kwangu.
Nilishusha
pumzi huku nikiongeza umakini wa kumsikiliza. Nilizidi kuwa katika wakati mgumu
kwa kujua kwamba kama nitamuendekeza sana msichana huyo basi pepo ya Mwenyezi
Mungu nitakuwa nimeipa kisogo.
Hata
hivyo nilijiambia ngoja kwanza nimsikilize, uamuzi si ulikuwa ni wangu bwana,
kama ningetaka kukubali basi ningekubali na kama ningetaka kukataa basi
ningekataa.
“Najua
mwanzo ulikuwa ukinichukia sana, hasa hasa pale niliposimama mbele ya mahakama
kutoa ushahidi juu ya kesi yako. Lakini sasa hivi hunichukii tena, hasa baada
ya kukuokoa kutoka kwenye kunyongwa, uongo?”
“Ni kweli.”
“Mateso yote uliyokuwa ukiyapata tangu kifo
cha marehemu kaka yako ulikuwa ukitumikia adhabu.”
Maneno
hayo yalinishtua na kunifanya nigutuke.
“Adhabu! Adhabu kwa kosa lipi? Na kosa hilo
nilikuwa nimemkosea nani?” Niliuliza.
“Kosa hukutenda wewe bali ni kaka yako James.”
“Alitenda kosa gani kaka yangu?”
“Usiwe na pupa, nipo hapa kukufunulia kila
kitu hivyo nitakueleza siri nzito aliyokuwa nayo kaka yako.”
Hilo
nalo lilikuwa neno; kujua kile kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia wakati wa
uhai wa kaka James, nilizidi kuongeza umakini. Kikao chetu kilizidi kutia fora,
sasa nikawa na shauku ya mambo matatu. Jambo la kwanza ni shauku ya kujua siri
nzito iliyokuwepo kwa kaka James.
Jambo
la pili lilikuwa ni shauku ya kujua masharti ambayo nilikuwa nimeambiwa
nitapewa wakati natoroshwa gerezani. Jambi la tatu ni shauku ya kutaka kujua
madhara yatakayonipata endapo ningeshindwa kutekeleza masharti hayo.
Sharifa
alianza kunieleza habari ya kaka James. Habari ambayo iliyaamsha machungu ya
moyo wangu, nikahisi maumivu makali yakipenya barabara kunako mtima wa moyo
wangu.
Kaka
James alipokuwa anamalizia masomo yake ya kidato cha nne aliambiwa na rafiki
yake mmoja kuwa kuna mganga wa kikongo aliyekuwa kaingia nchini. Mganga huyo
alikuwa akiwatengenezea watu dawa ya kupata utajiri.
Kutokana
na tamaa za kutaka kupata utajiri, kaka James alimtaka rafiki yake huyo
ampeleke kwa mganga huyo ili akatengenezewe dawa ya kuwa tajiri. Ndipo
alipopelekwa.
Alipofika
kwa mganga huyo aliambiwa kuwa masharti ya kupata utajiri ni lazima uingie
maagano na majini. Maagano hayo yalikuwa ni maagano ya kafara za damu huku
yakiwa katika madaraja matatu.
Daraja la kwanza
lilikuwa ni kuwatoa kafara wazazi wako wote pamoja na ndugu yako mmoja wa damu.
Ndugu aliyetakiwa katika daraja hili ni mdogo wako, kaka yako ama dada yako.
Kama wote hao huna basi mjomba ama shangazi hutakiwa.
Baada ya hapo utajiri
unaanza kwa kasi ya kawaida. Ukishakaa miaka mitano unatakiwa kutoa tena kafara
ya mtoto wako wa kwanza pamoja na mama yake kama wewe ni mwanaume. Lakini kama
ni mwanamke basi unatakiwa kumtoa mtoto wako wa kwanza pamoja na baba yake.
Ukishakamilisha
kafara za daraja la kwanza na la pili unatakiwa sasa kuhamia kwenye daraja la
tatu ambalo kafara yake huendelea mwaka hadi mwaka. Kafara katika daraja hili
ni ya mtu yeyote ama awe mfanyakazi wako au anayetumia vitu vyako mfano abiria
katika magari yako, mpangaji katika nyumba yako na kadhalika.
Masharti
hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia
kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika
ajali ya kutisha.
HAYA SASA, MAMBO NDO YANAFIKIA
PENYEWE, NINI KITATOKEA? USIKOSE TOLEO LIJALO!
Wednesday, December 4, 2013
MIRATHI YA KAKA toleo la 51
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Alirudi
ndani haraka huku akiwa na hasira kisha akaufunga mlango kwa kuukomea ili
kumkomoa mtu aliyekuwa akileta ubishi pale mlangoni. Sikutaka kumuuliza
chochote kwani kama ningeongea basi sauti yangu ingesikika na kisha mpango wetu
kubumbuluka.
SASA ENDELEA..........
Alijitupia kitandani
huku akimlaumu mwanamke huyo kwa kuwa mbishi bila sababu. Huku akiwa bado
analalama, tuliuona mlango ukifunguka licha ya kukomea wakati anaufunga.
Pamoja na ubabe aliokuwa nao Benja alijikuta
akinywea baada ya kuona mlango unafunguka. Hakuendelea tena kubwabwaja badala
yake alibaki mdomo wazi huku hofu na woga vikimjaa.
Baada ya mlango
kufunguka msichana aliyekuwa anabishana na Benja mlangoni aliingia mpaka
chumbani. Kumbe alikuwa ni Sharifa, msichana aliyekuwa kanisababishia kufungwa
kisha kuniokoa dakika chache kabla ya kunyongwa kitanzini.
Sasa nilikuwa
nimeshaanza kumzoea msichana huyo.
“Ooh! Sharifa, kumbe ni wewe, samahani kwa
yote yaliyojitokeza kwani mwenzio nalazimika kuishi kama digidigi.” Nilimwambia
huku nikimlaki kwa kumkumbatia.
Wakati
huo Benja alikuwa aking’aang’aa sharubu tu, nikamtambulisha kwa Sharifa huku
tukiwa bado tumekumbatiana. Alishusha pumzi kwa nguvu na kurudi katika hali
yake ya kawaida.
“Mbona
unaishi kwa woga na wasiwasi hivi?” Sharifa alinitwanga swali hilo.
“Naogopa kugundulika kuwa nimetoroka jela,
maana jambo hilo tulilifanya tu kwa uwezo wako ila ni la hatari mno.” Nilijibu vile.
“Wasiwasi wako tu. Hakuna mtu yeyote
atakayekuuliza juu ya hilo hata kama uende gerezani hapo hapo.” Aliongea tena
Sharifa kunitoa wasiwasi.
Hata
hivyo maneno yake sikuyasadiki hata kidogo ila nilikubali ili yaishe.
Nilipomuomba tukae japo pale kwenye godoro ili anisaidie ushauri juu ya suala
lililokuwa linaumiza kichwa changu
alikataa. Akasema alikuwa amekuja kunichukua ili tuende kumalizia
maongezi yetu tuliyokuwa tumeyabakisha kule gerezani kabla ya kutoroka.
Nilipomuuliza
tunaenda kuongelea wapi aliniambia anajua yeye, nilichokuwa natakiwa kufanya ni
kumfuata kokote ambako ataniambia tuende.
Nilimuaga
Benja kisha tukaondoka na Sharifa. Sikuwa na nijualo juu ya safari hiyo. Tulipotoka nje ya nyumba alimokuwa kapanga
Benja tuliingia kwenye gari moja la kifahari ambalo alikuwa amekuja nalo
msichana huyo. Safari ya kuelekea nisikokujua ilianza huku dreva akiwa ni yeye.
Baada
kama ya nusu saa tulikuwa tupo kwenye hoteli moja mashuhuri sana mjini hapo.
Hoteli hiyo ilikuwa siyo ngeni kwangu japokuwa nilikuwa sijawahi kuingia ndani
zaidi ya kuliona jengo lake kwa nje nikiwa napita karibu nayo.
Wakati
tunashuka kwenye gari hiyo mara baada ya kufika hotelini hapo, Sharifa
alichukua ‘brificase’ na kushuka nayo akiwa kaishikilia mkononi.
Sikuelewa
kama tayari alikuwa kashalipia chumba au vipi kwa sababu tulipapita mapokezi
bila kusimama, tukaenda moja kwa moja kwenye lift. Tulipofika lift
ikatupandisha mpaka ghorofa ya saba, tukatembea kwenye korido mpaka kwenye
chumba namba 138.
Tulipofika
kwenye chumba hicho Sharifa alifungua mlango kwa kadi maalumu nao ukafunguka
kisha tukazama ndani. Chumba kilikuwa matawi ya juu kweli kweli, kila huduma
inayopatikana kwenye vyumba vya hoteli kubwa kubwa basi hata humo ilikuwepo.
Kimawazo
nilikuwa mbali sana wakati huo. Akili yangu ilikuwa inazunguka kuwaza ni
masharti gani nitapewa na msichana huyo ikiwa ni malipo ya kuniokoa kutoka
kwenye kunyongwa kwa kitanzi.
Mwili
wangu ulikuwa umezizima mithili ya mtu aliyetota kwa kunyeshewa mvua. Nilikuwa
mdogo kama pilton.
Tulipoingia
tulikaa kwenye sofa za nguvu, ndipo mazungumzo yetu yalipoanza.
“Brighton mwana wa David!” Sharifa alichokoza
mada kwa kuanza kuniita.
“Naam!” Niliitikia na kukaa kimya kusikilizia
kitachachoongewa.
“Bila shaka unapenda sana kuwa tajiri, maana umekuwa
ni mtu mwenye kujituma na kujishughulisha ukiwa na lengo la kuusaka utajiri!
Kweli ama si kweli?”
“Ni kweli, lakini utajiri ninaopenda mimi ni
ule wa kuupata kwa njia za halali zenye kumpendeza Mungu.”
Baada
ya kujibu hivyo nilimuona Sharifa akiangua kicheko cha dharau kisha akaendelea
kusema,
“hayo ni mawazo finyu ambayo hayataleta tija
katika maisha yako. Utajiri hauji kwa njia za halali hata siku moja na Mungu
hawezi akakuletea utajiri. Tangu lini kitu haramu kikaja kwa njia halali?”
Kauli
hiyo iliniacha njiapanda kidogo. Ikanifanya nirejee kwenye mafundisho ya dini
niliyoyapata nikiwa bado kinda wakati huo, mafundisho yaliyozungumzia matajiri
wa kale ambao miongoni mwao ni kina Ibrahim na kina Ayubu, mbona wao walikuwa
ni wacha Mungu wazuri tu?
Nikakumbuka
tena maneno ya Yesu kristo alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake kuwa ni vigumu
kwa tajiri kuingia kwenye ufalme wa Mungu kuliko hata kwa ngamia kupenya katika
tundu la sindano.
‘Je, maneno haya huenda ndiyo yanaashiria
anachokisema Sharifa?’ nilimalizia tafakuli yangu kisha nikatoa jibu kuwa si
matajiri wote wanaoupata utajiri kwa njia za mkato.
“Tuendelee!”
niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu, hivyo kama
unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali nitakayokuambia.”
Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua brificase iliyokuwa
mezani.
JE, NI MAMBO GANI BRIGHTON
ATAAMBIWA NA SHARIFA AMBAYO YATAMFANYA AWE TAJIRI? USIKOSE TOLEO LIJALO!
Sunday, December 1, 2013
MIRATHI YA KAKA sehemu ya 50
KWA WASOMAJI WAPYA......
Brighton anaota ndoto ya ajabu
akiwaona watu waliokufa siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick,
James na Anna. Baada ya ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa
anayemsababishia kesi ya mauaji ya mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi
inaunguruma mahakamani kisha anajikuta akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka
afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa
gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa
amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James, naye Mack anaanza kumhadithia kisa
kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. Hatimaye siku ya kunyongwa inafika kweli, hata
hivyo anajikuta anakolewa kimiujiza na msichana aliyemsingizia kuua, yaani
Sharifa, anatolewa gerezani na kuwa huru kabisa.
Anaporudi
kwake anakuta nyumba yake ishauzwa na mtu aliyekuwa amemwachia. Anaamua kwenda kwa jamaa yake na huyo mtu
kumuulizia naye anaambiwa jamaa huyo katimkia Afrika ya kusini.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Nilipomaliza kula
mazungumzo yalianza. Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kusikia habari za Mapara.
Hata hivyo kwa wakati huo nilikuwa na uhakika wa kusikia habari zote za Mapara
kutoka kwa Benja kwani ukaribu wao ulikuwa ni kama pete na chanda.
SASA ENDELEA..........
Alianza kwa kunipa pole kwa matatizo yote
yaliyokuwa yamenisibu. Baada ya hapo alianza kunieleza habari niliyokuwa
naingijea kwa hamu kubwa.
“Tangu
upatwe na matatizo Mapara alikuwa akijitahidi sana kuisimamia miradi yako. Tena
ilikuwa ikiendelea vizuri kila kukicha.” Alinieleza Benja.
Wakati
huo nilikuwa makini kusikiliza; hatua kwa hatua, neno kwa neno huku nikiwa na
maswali tele kichwani juu ya hatima ya mali zangu baada ya kudokezwa kuwa
niliyekuwa nimemwachia dhamana ya kuziangalia na kuzitunza alikuwa katimkia
ughaibuni.
Benja
aliendelea kunieleza kuwa baada ya hukumu yangu Mapara alianza kujitapa kuwa
mali zote hizo nilikuwa nimemkabidhi. Akawa na jeuri ya pesa kupindukia, si
unajua tena baadhi ya watu wanapopata pesa kirahisi rahisi huwa hawana machungu
nazo!
Akawa
ni mtu wa ahasa. Wanawake na yeye, tena akawa anawabadilisha kama nguo. Mchana
yupo na huyu, asubuhi alikuwa na yule na usiku utamuona na mwingine. Pombe na
yeye kila wakati.
Baada
ya kutapanya mali kwa miezi kadhaa uchumi wa miradi yangu ulianza kushuka.
Ndipo alipoanza kuuza kila kitu ili atimkie Bondeni kwa mzee Madiba, yaani
Afrika ya kusini.
Alimalizia
kwa kuuza nyumba yangu akamuuzia kigogo mmoja ambaye alikuwa ni mbunge. Baada
ya kukamilisha uuzaji wa nyumba yangu Mapara alikwea ‘pipa’ na kuishia ‘Sauzi’.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa habari ya Mapara kwa mujibu wa maelezo ya Benja.
Kichwa
changu kilizidi kuwa kizito utadhani kilikuwa kimeng’atwa na manyigu.
Sikutegemea kabisa kama Mapara angefanya utumbo kama ule.
Mpaka
hapo mipango yangu yote ilikuwa imechemka, kwa msemo wa vijana wa kileo ilikuwa
‘imebuma’. Niliendelea kupiga miayo mfululizo utadhani sijala siku tatu wakati
ndiyo nilikuwa nimemaliza kushindilia sahani ya ubwabwa..
“Sasa
utanisaidiaje rafiki yangu, maana sitaki kabisa kuendelea kuishi kwenye mji huu
kwani watu wanaweza wakasanua ishu kuwa nimetoroka jela.” Nilimuuliza Benja kwa
sauti ya huruma.
“Kwa hiyo unataka ukaishi mji upi?”
“Mji wowote ule ilmradi uwe upo mbali na huu,
nchi yetu ina miji mingi tu ambayo shughuli za kiuchumi zinapatikana. Nina
imani nikifika sehemu na kutulia baada ya muda fulani mambo yangu yatakaa
sawa.” Nilizidi kumweleza Benja.
Pamoja
na kuwa nilikuwa nipo mikononi mwake nikiamini kabisa kuwa shida yangu
itafanikiwa, mambo yalizidi kuwa si mambo. Msaada wake ulikuwa si zaidi ya
kunihifadhi kwa siku kadhaa ambazo ningekaa kwake. Kuhusu suala la pesa alikuwa
ni mtupu.
Sikushangaa
kusikia hivyo kwa kijana huyo kwani tangu sijaenda jela maisha yake yalikuwa
yapo vilevile. Pamoja na kukaa miaka lukuki jela bado nilimkuta hajaongeza hata
stuli kwenye chumba chake hicho zaidi ya godoro la kulalia na redio kaseti
aliyokuwa nayo.
Hii
yote ilitokana na kutojishughulisha katika maisha yake. Si yeye peke yake bali
kulikuwa na vijana wengi tu katika mji huo waliokuwa na kasumba ya
kukusanyikana kwenye masikani zao tu na kuanza kucheza kamali kutwa nzima.
Baada
ya kukosa msaada kwa mwenyeji wangu huyo nilikaa kimya kama dakika kumi hivi
nikitafakari la kufanya ili kukimbilia kujificha kwenye mji mwingine tofauti na
huo. Mapara alikuwa kashaniponza kwa kuyapeleka kombo mambo yangu yote.
Kabla
hatujafikia muafaka juu ya sakata langu, mlango wa chumba cha Benja uligongwa.
Moyo wangu ulilipuka ‘lipu’ huku hofu ya kukamatwa ikitanda katika mawazo
yangu.
Naye Benja aliinuka
taratibu na kwenda kufungua mlango kidogo kidogo kisha akatoka kumsikiliza
aliyekuwa anagonga.
Sauti ya msichana
niliisikia ikimsalimia Benja kisha kumhoji ikimuuliza kama nilikuwemo ndani.
Mapigo ya moyo yalizidi kwenda kasi baada ya kusikia jina la Brighton
likitajwa, yaani jina langu.
Ilikuwa hainipi
kabisa akilini kwa mtu mwingine yeyote katika mtaa huo au mji kwa ujumla kujua
kuwa nilikuwa nimetoka jela. Sasa kitendo cha mtu kuja moja kwa moja na kugonga
nilipokuwa nimefikia kisha kuniuliza kilikuwa kimenikosesha kabisa amani
moyoni.
Nilibaki nikiomba
kimungu mungu wasije wakawa askari polisi ama wana usalama. Nilijikuta
nikiogopa hata kupumua kwa kuhofia mihemo yangu kusikika huko nje ya chumba.
Mara nilimsikia Benja
akimhoji mtu aliyekuwa akiniulizia kuwa ni nani na alikuwa akinitafutia nini.
Hata hivyo majibu ya msichana huyo sikuyasikia kwani alikuwa akiongea polepole
sana.
“Huyo Brighton
unayemuulizia haishi hapa wala mimi simjui. Kwanza hilo jina ni geni kabisa
katika mtaa wetu, kama vipi endelea kuulizia kwa wengine.” Nilimsikia Benja
akijibu hivyo.
Moyo wangu ulifurahi
sana kusikia Benja akijaribu kupapatua ili kuokoa maisha ya uhai wangu uliokuwa
umebaki. Hata hivyo mabishano makali yaliibuka baina ya mwanadada huyo na
Benja.
Mwanadada huyo
alikuwa akidai kuwa ana uhakika wa asilimia mia moja kuwa nilikuwemo chumbani
humo huku Benja yeye akikanusha vikali.
Alirudi ndani haraka
huku akiwa na hasira kisha akaufunga mlango kwa kuukomea ili kumkomoa mtu
aliyekuwa akileta ubishi pale mlangoni. Sikutaka kumuuliza chochote kwani kama
ningeongea basi sauti yangu ingesikika na kisha mpango wetu kubumbuluka.
HUYU MWANAMKE NAYE SASA ANATAKA
KULETA BALAA KWA BRIGHTON! JE, NI NANI HUYO NA ANASHIDA GANI NA BRIGHTON?
Subscribe to:
Posts (Atom)