Brighton anaota ndoto ya ajabu
akiwaona watu waliokufa siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick,
James na Anna. Baada ya ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa
anayemsababishia kesi ya mauaji ya mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi
inaunguruma mahakamani kisha anajikuta akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka
afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa
gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa
amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James, naye Mack anaanza kumhadithia kisa
kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. Hatimaye siku ya kunyongwa inafika kweli, hata
hivyo anajikuta anakolewa kimiujiza na msichana aliyemsingizia kuua, yaani
Sharifa, anatolewa gerezani na kuwa huru kabisa.
Anaporudi
kwake anakuta nyumba yake ishauzwa na mtu aliyekuwa amemwachia. Sasa endelea...................
Wakati nagonga wimbo
uliokuwa unakita ulifikia mwisho, hapo hapo na mimi nikagandamizia kuendelea
kugonga ili nipate kusikika. Kabla wimbo mwingine haujaanza kusikika niliweza
kuona mlango ukifungulia. Ndipo alipotoka kijana ambaye nilikuwa namfahamu; alikuwa
akiitwa Benja.
Hata
hivyo hakuonyesha dalili zozote za kuweza kunitambua. Nilikuwa nimebadilika si
mchezo. Sikuwa kama Brighton wa kipindi kile, enzi hizo kina Mapara na hao kina
Benja walikuwa wanapenda kuniita pedeshee mtoto, jina ambalo nilikuwa nalipinga
vikali kwani nilikuwa sipendi majisifu.
Nilipogundua
kwamba hajanifahamu nilianza kujiuliza,
‘Sijui nimkumbushe, sijui nijikaushe tu ili
siri yangu izidi kudumu. Lakini nikijikausha atanipa michapo yote kuhusu
Mapara?” Nilizidi kuwaza na kuwazua wakati tukisalimiana.
Suala
la kujikausha ndilo lililopitishwa na halmashauri ya ubongo wangu japokuwa kama
angekuwa mgumu kunieleza habari nilizokuwa nazihitaji basi ningejifunua kwake.
Baada
ya salamu mazungumzo yaliendelea,
“Karibu bwana!”
“Asante!”
“Karibu pita ndani.”
“Asante lakini nipo haste haste kidogo,
namulizia Mapara.”
“Unamuulizia Mapara?”
“Ndiyo!”
“Ni nani yako huyo Mapara?”
“Ni rafiki yangu!”
“Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni lini?”
“Ni miaka mingi kidogo lakini sikumbuki”
Maswali
ya Benja aliyokuwa akiuliza mfululizo utadhani naye ni polisi yalianza
kunikera. Hata hivyo niliona nikianza kumjibu utumbo sitafanikisha nilichokuwa
nakihitaji. Nililazimika kuwa mpole kama simba jike anapozaa ili nifanikishe
suala langu, suala la kupata habari za Mapara.
Niliendelea
kjitahidi kumjibu kila swali alilouliza.
“Wewe ni mwenyeji wa wapi?”
“Ni mwenyeji wa mji huu huu ila nilisafiri
siku nyingi.”
“Dah! Huyu Mapara ana miaka mingi sana hayupo
nchi hii!”
“Yupo nchi gani sasa?”
“Hata mimi sijui ila ninachojua ni kwamba
huwezi ukampata mji huu wala nchi hii.”
Mpaka
hapo nilikuwa nimeishiwa maji. Mambo yalizidi kuniwia ugumu baada ya kuambiwa
kuwa Mapara alikuwa yupo nchi za ng’ambo.
Hata
hivyo nilijua dhahiri ya kwamba Benja alikuwa ananificha kunieleza habari
kamili. Niliamini kabisa kuwa alikuwa anajua mambo mengi sana kuhusu Mapara
kwani alikuwa ni mtu wake wa karibu sana.
Baada
ya kuona mambo yamenikaa vibaya sikuwa na budi kunyolewa. Nilimuomba Benja
tuingie ndani kwake ili nikamuelezee matatizo yangu kwani nilikuwa na matatizo
makubwa.
Benja
hakukataa. Alinikaribisha ndani nami nikaingia. Tulipofika ndani nilimweleza
kinaga ubaga bila kumficha kitu chochote kuhusu kesi yangu ilivyoenda, hukumu
mpaka kutoroka kwangu siku hiyo ambayo ilikuwa ndiyo siku ya kunyongwa.
Alistaajabu
sana kusikia hivyo.
“Unajua nilikuwa nakufananisha kwa mbaali
lakini nikawa najiambia mwenyewe itawezekanaje mtu aliyehukumiwa kunyongwa
aonekane tena uraiani? Na ingekuwa kwa msamaha wa rais basi tungesikia kwenye
vyombo vya habari.”
Kabla
hatujaanza hata maongezi yetu Benja aliniambia nimsubiri kidogo, alitoka nje na
kwenda sehemu ambapo sikukujua. Huku nikiwa ndani niliendelea kusikiliza nyimbo
za mziki wa kizazi kipya ambao niliuacha ndiyo kwanza unachipuka.
Hata
hivyo nilihisi mabadiliko makubwa sana kwenye mziki huo kwani nyimbo zilikuwa
na ubora wa hali ya juu kushinda enzi zile bado sijafungwa. Kweli kuwa jela ni
sawa na kutokuwa kwenye hii dunia kwani unakuwa hujui kinachoendelea uraiani.
Baada
ya muda usiozidi nusu saa niliona mlango ukifunguliwa, ndipo alipotokea Benja
akiwa na kifuko kaning’iniza ambamo kulikuwa na chakula.
Alinitengea
nami nikaanza kula. Kusema kweli nilikuwa na njaa ya kufa mtu. Tumbo nilikuwa
likisokota kwa njaa si mchezo. Nilianza kula chakula kilichokuwa kimeletwa na
Benja kutoka mkahawani.
Nilipomaliza
kula mazungumzo yalianza. Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kusikia habari za
Mapara. Hata hivyo kwa wakati huo nilikuwa na uhakika wa kusikia habari zote za
Mapara kutoka kwa Benja kwani ukaribu wao ulikuwa ni kama pete na chanda.
JE, BRIGHTON ATAAMBIWA HABARI GANI
ZA MAPARA NA MWENYEJI WAKE BENJA? JIBU LIPO TOLEO LIJALO.