Wednesday, October 30, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 38


ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Baada ya kuwaza kidogo alikumbuka kuwa bastola yake ilikuwa imebakiza risasi moja ndani. Ndipo alipoamua kujimaliza na yeye kwa kujipiga risasi.
SASA ENDELEA.......
Wakati huo nilikuwa namfuatilia kwani machale yangu yalikuwa yamenicheza. Wakati anaondoka nyumbani alikuwa kashaniambia kuwa anaenda kwa mpenzi wake ila alikuwa akienda bila ya taarifa huku akiyavunja masharti aliyokuwa amepewa na mpenzi wake huyo. 
Niliamua kumfuatilia ili nikashuhudie ‘timbwilitimbwili’ nililokuwa nikilitegemea kuibuka baada ya kaka James kufika kwa mpenzi wake huyo. Hata kama yangetokea mapigano kisha kaka yangu akazidiwa basi mimi ningekuwepo nyuma yake kuokoa jahazi.
Hata hivyo aliniacha njiani kwani alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi mno. Mimi nilikuwa naogopa ajali hivyo nikawa naendesha mwendo wa kistaarabu.
Kwenda kwangu polepole ndiyo kulinifanya nimkose kaka James katika dunia hii kwani nilichelewa kiduchu mno. Wakati naufikia mlango wa chumba walichokuwamo kina Neila, tayari kaka James alikuwa kashakitekenya kitufe cha kufyatulia risasi huku akiwa amejilenga kwenye kichwa chake.
Nilimshuhudia kaka James akianguka mzima mzima kisha akakata roho. Ndipo nilipopoteza fahamu na kushindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.
Fahamu zilinijia masaa matano mara baada ya tukio hilo kutokea. Nilijikuta nipo wodini huku nikiwa nimetundikiwa drip ya maji. Nilishangaa sana kujikuta nipo hospitali.
Katika kuvuta kumbukumbu nilikumbuka jinsi mambo yalivyokuwa masaa matano yaliyokuwa yamepita. Nilikumbuka kuwa kaka James hakuwepo tena duniani.
Nilizidi kuchanganyikiwa, akili yangu ikazidi kuvurugika baada ya kukumbuka hilo tukio lililokuwa na tanzia kubwa katika moyo wangu na akili yangu kwa ujumla.
Sikuona kabisa mantiki ya kuendelea kubaki hospitali wakati nyumbani kulikuwa na msiba wa marehemu kaka yangu. Sikujua ni vipi mipango ya mazishi ilikuwa inapangwa huko kwani mimi ndiyo nilikuwa ndugu wa pekee wa marehemu. Kwa kifupi mhusika mkuu wa msiba huo nilkuwa ni mimi.
Nilipojaribu kuangaza angaza niliona karibu wagonjwa wote wamelala kwenye vitanda vyao kila mmoja. Sikuona muuguzi wala dakitari yeyote aliyekuwemo kwenye wodi hiyo.
Bila kuchelewa wala kuduwaa niliichomoa sindano ya drip na kutoka mbio kuelekea nyumbani kuungana na majirani kuomboleza kifo cha kaka James.
Kwa vile James alikuwa mtu mashuhuri sana katika mji huo, tayari taarifa za kifo chake zilikuwa zimeshazagaa mtaani na katika mji wote kwa ujumla.
Nilipofika nyumbani niliwakuta watu wengi wameshakusanyika. Hata hivyo mwili wa marehemu ulikuwa upo hospitali umehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi. Nilijumuika na watu waliokuwa wameshafika, maombolezo yakaendelea.
Watu walizidi kumiminika kuja kunipa faraja kwenye msiba huo. James alikuwa ni mtu wa watu, alijua kukaa vizuri na majirani pamoja na watu wengine aliokuwa akifahamiana nao. Hali ya watu kujaa ilinifariji kwa kiasi fulani ingawaje moyo wangu ulikuwa umeghubikwa na majonzi yasiyokuwa kifani.

            ******************************

ITAENDELEA....

Monday, October 28, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 37



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Mpaka namaliza kidato cha sita alikuwa ni tajiri wa kuogopeka mji mzima. Alikuwa na magari mawili ya kifahari na nyumba mbili za kifahari.
SASA ENDELEA.......
Tulihamia kwenye nyumba moja na kuanza kuishi pale. Mambo yalizidi kuwa safi kwa kaka James. Nilizidi kupata wasiwasi kwa jinsi utajiri wake ulivyokuwa ukiongezeka kila kukicha.
Kati ya miradi mikubwa aliyokuwa nayo ni pamoja na kampuni ya usafirishaji ambayo ilikuwa na malori ya kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi. Ilikuwa ni kampuni kubwa iliyokuwa imeajiri wafanyakazi wengi mno.
                       
************************
           
            Mahusiano ya kimapenzi kati ya kaka James na mwanadada Neila yalizidi kupamba moto. Hapo awali mimi nilikuwa sijui chochote kuhusu uhusiano huo kwani alikuwa hajanitambulisha.
            Ilifikia kipindi akanitambulisha rasmi na kuniambia Neila ndiye alikuwa tashtiti wake, nyonga mkalia ini kama wasemavyo watu waliobobea kwenye mahaba.
            Sikuwa na pingamizi juu ya uhusiano wao ila niliwasisitiza tu watangulize uaminifu mbele pamoja na upendo wa dhati kwa ujumla.
            Mapenzi yao yaliendelea kukolea kila siku iliyoenda kwa Mungu. Hapo ndipo Naila alianza katabia ka kudai makuu ikiwemo kukabidhiwa nyumba kununuliwa gari zuri la kifahari pamoja na kufunguliwa akaunti yenye hale nyingi.
Hayo yote hayakuwa tatizo kwa kaka James maana pesa ilikuwa chekwa. Kila alichotaka mtoto wa watu alitimiziwa, mpaka nikaanza kumuonea wivu kwani alizidi mno kumpiga ‘kibomu’ kaka yangu. Naye James kwa kutaka kumkoleza mwanadada huyo hakuona ajabu kuvitoa vimilioni kwa ajili yake.
            Siku chache baada ya kaka James kumkamilishia mambo hayo; mwanamke huyo alibadilika ghafla na kuanza kufanya vimbwanga vilivyokuwa vikileta kichefuchefu mbele ya James.
            Tabia ya mwanamke huyo ilizidi kuwa mbaya, akawa anamletea kiburi kaka yangu huku akimpa masharti mengimengi ikiwa ni pamoja na kuwa anatoa taarifa akitaka kwenda kwake.
            Siku moja kaka James alienda kwa mwanamke huyo bila taarifa. Alichokikuta huko hakuamini kwa macho yake kwani alikikuta kidume kimejilaza kitandani kikiwa na mwanamke huyo huku wakiwa kwenye pozi la kimahaba.
            Ghadhabu zilimjaa sana kaka James baada ya kuyashuhudia yale mambo.
“Nini hicho unafanya mpenzi wangu?” Alisikika James kwa sauti ya kitetemeshi akionyesha ni jinsi gani hasira ilivyokuwa imepanda.
“Nani mpenzi wako?” Aliuliza mwanamke huyo kwa jeuri na nyodo za kila aina.
Kauli hiyo ilizidi kuipandisha hasira ya James. Hapo ndiyo alipojua ya kwamba mwanamke huyo ni nyoka ndumilakuwili mwenye sumu kali.
“Sikia nikwambie James; kama kusoma hujui basi jaribu hata kuangalia picha! Wewe ni zilipendwa ndugu yangu, tangu lini mavi ya kale yakanuka?. Mwanaume mwenyewe upo kianalojia utarandana vipi na mimi nipo kidigitali zaidi? Sasa nakutangazia rasmi leo kuwa sikupendi na sikuhitaji, na huyu unayemuona hapa ndiye mwanaume ninayempenda kwa dhati ambaye anastahili kuniona. Upo hapo? Hii ndiyo habari ya mjini babu wee!” Alizidi kutamba mwanamke huyo kisha akamalizia kicheko cha kishambenga,
“Heheheeeyah!”
“Kefle! Unajifanya mjanja na kuniona bwege mimi, sasa anza kusali sala zako za mwisho kwani uhai wako naukatisha sasa hivi?” Alidakia James kwa sauti ya juu iliyowashitua Neila na jamaa yake aliyekuwemo humo ndani.
Siyo sauti ya juu pekee iliyowafanya waduwae bali ni pamoja kitu alichokuwa amekishika mkononi. Kitu hicho hakikuwa kingine bali ni kidubwasha mithili ya kipaja cha kuku kilichoundwa kwa madini shaba. Alikuwa ameshika bastola.
Mwanamke yule alianza kutetemeka na kuanza kuomba msamaha kwa James, kwa bahati mbaya alikuwa amechelewa! Bila ya huruma James alikitekenya kitufe cha kufyatulia risasi kisha akamtwanga mwanamke huyo ya kichwa.
Huku akiwa anatweta kwa hasira aliisukuma risasi nyingine ambayo ilimpata yule jamaa aliyekuwa akijaribu kulamba asali kwenye mzinga wa James.
Risasi hiyo nayo ilimpata barabara kijana huyo, ikapenya kupitia kwenye paji lake la uso na kumfanya naye aanguke chini. Hakuchukua muda akawa amerudisha jezi ya kuendelea kuishi kwa mwenyezi Mungu, ikawa ni kwa heri mwalimu!
Mpaka hapo dhambi ya mauaji ya watu wawili kwa mpigo ilianza kumtafuna kaka James. Hofu na woga vilitanda katika moyo wake, akaanza kuona kesi ya mauaji ya watu wawili ilikuwa inamkabili.
Baada ya kuwaza kidogo alikumbuka kuwa bastola yake ilikuwa imebakiza risasi moja ndani. Ndipo alipoamua kujimaliza na yeye kwa kujipiga risasi.
ITAENDELEA....

Saturday, October 26, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 36

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Kuzaliwa kwa kaka James ndiyo kulikuwa hivyo. Wakati huo mimi nilikuwa bado sijafikiriwa hata kuiona hii dunia. Nilikuwa bado nipo mbinguni nikicheza na kufurahia tu na malaika.
SASA ENDELEA.......
Baada ya kujifungua mama yangu hakupata tena nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kwani huo mfumo umekuja miaka ya hivi karibuni. Zamani ukinasa huku bado unasoma basi hiyo ndiyo nitolee tena.
Haikuwa kama siku hizi ambapo msichana akipata mimba yungali anasoma anaruhusiwa kwenda kuilea mimba kisha akishajifungua anaendelea na masomo. Miaka ile haikuwa hivyo.
Hata hivyo mama yangu alikuja kujiunga na ualimu wa UPE enzi zile rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hayati Mwl. Julias Kambarage Nyerere alipotangaza elimu ya UPE.
Kwa wale wenzangu na mimi ambao wamezaliwa juzijuzi  kuelekea kwenye mfumo wa digitali, maana ya UPE ni mpango ulioanzishwa na aliyekuwa rais wa kipindi hicho hayati Baba wa taifa Mwl. Nyerere ambao ulitaka kila mtoto wa kitanzania asome elimu ya shule ya msingi.
Hapo ndipo ulipotokea upungufu mkubwa wa walimu wa shule za msingi kiasi kwamba walimu waliokuwa wametoka vyuoni wakawa hawakidhi mahitaji.
Ndipo serikali ilipotangaza nafasi za ualimu hata kwa wale waliokuwa wameishia njiani na kushindwa kumaliza kidato cha nne pamoja na wale waliokuwa wamemaliza darasa ya saba nao walichukuliwa na kupewa jukumu ya kuwa walimu.
Kati ya hao walimu wa UPE na mama yangu naye alibahatika kuwamo. Akawa amepangiwa shule ya kufundisha.
Ilipita miaka kadhaa. Huku akiwa mwalimu alipata mume na kumuoa. Ndipo nilipozaliwa mimi.
Wakati huo kaka James alikuwa akiishi na wazazi wake na mama, yaani namaanisha kwa bibi na babu. Mpaka walipokuja kufariki ndipo alipochukuliwa na mama na kukaa pamoja katika familia moja.
Baba yangu alimchukulia kaka James kama alivyokuwa akinichukulia mimi, yaani alimlea kama mwanae wa kumzaa wakati alikuwa ni baba yake wa kufikia.
Hapakuwa na ukambo ukambo hapo, baba yangu alikuwa kapenda boga pamoja na maua yake. Alikuwa tofauti kabisa na baadhi ya wanaume ama wanawake wengine wanaowachukia watoto wa kambo.
Kama zawadi alituletea wote bila ya upendeleo, kama adhabu alitoa bila ya kupendelea, kama ni mapenzi basi alitupatia mapenzi mema wote wawili.
Kaka James hakuwahi kuwa na upweke kwa kulelewa na baba wa kambo. Alikuwa akithaminiwa kama kawaida, hakika maisha yake yalikuwa ni ya furaha siku zote.
Nadhani upendo tuliokuwa tukiupata kutoka kwa baba na mama ndiyo ulioimarisha uhusiano wetu na udugu wetu uliokuwa wa kushibana kama vile mapacha.
Hata hivyo furaha yetu ilikuja kubadilika na kuwa majonzi pale wazazi wetu walipokuja kupata ajari mbaya ya gari na kupoteza maisha papo hapo. Vifo vya wazazi wetu kwa mkupuo vilichimba donda kumbwa mno moyoni mwangu.
Usiombe ndugu msomaji kuwapoteza wazazi wako kwa wakati mmoja, maumivu yake ni zaidi ya msumari wa moto ukandamizwapo kwenye kidonda kinachoelekea kupona.
Tukio hilo huwa sipendi hata kulielezea kwani huwa linaibua machungu makubwa mno ndani ya moyo wangu. Yaani wee acha tu. Kama ukitaka nianze kububujikwa na machozi basi nikumbushie tukio hilo tu, aisee! Bora niachane na hizo habari kwani zitanifanya nishindwe hata kuendelea kukuhadithia yanayohusu mirathi ya kaka.
Wakati wazazi wetu wanatutoka mimi nilikuwa nipo darasa la tatu na kaka James alikuwa ndiyo kahitimu kidato cha nne.
Mara baada tu ya wazazi wetu kufariki kaka James alitaka tugawane mali tulizokuwa tumeachiwa. Kwa kuwa mimi nilikuwa mdogo sana, sikuwa na la kuamua wala kushauri zaidi ya kuwa kama bendera nikifata maamuzi ya kaka yangu.
Tuligawana mali zote huku nyumba akiniachia mimi. Hata hivyo tuliendelea kuishi hapo wote licha ya nyumba kuwa mikononi mwangu. Baadhi ya mali  nilizokuwa nimegawiwa kutoka kwenye mirathi hiyo tuliziuza ili zinisaidie katika masomo.
Kaka James yeye aliuza kila kitu, lakini hakutaka tena kuendelea na shule badala yake alianza kufanya biashara huku akiwa na mtaji wa kutosha kutokana na kuuza mirathi yake yote.
 Nilifanikiwa kusoma mpaka kidato cha sita huku kaka yangu yeye akiishia kidato cha nne tu. Lakini mpaka namaliza shule mwenzangu alikuwa kashakuwa tajiri huku biashara zake zikishamiri vizuri.
Kasi ya kupata utajiri kwa kaka James ilikuwa kubwa sana mpaka nikaanza kushangaa. Nilipojaribu kumuuliza kaka James kulikoni naye aliniiambia ni baraka kutoka kwa Mungu. Hilo ndilo lilikuwa jibu lake pindi nilipomuuliza kuhusu utajiri huo aliokuwa akiupata kwa kasi.
Mpaka namaliza kidato cha sita alikuwa ni tajiri wa kuogopeka mji mzima. Alikuwa na magari mawili ya kifahari na nyumba mbili za kifahari.

ITAENDELEA......

Thursday, October 24, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 35



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Mpaka anafikishwa hospitali mama yangu alikuwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa kaumia vibaya sana

                        ************************
SASA ENDELEA.......
Taarifa za ajali ziliwafikia wazazi wa mama majira ya mchana, walipigiwa simu na mwalimu mkuu wa shule aliyokuwa akisoma mama na kuambiwa kuwa mtoto wao kapata ajali katika moja ya basi lililokuwa likienda mji jirani muda mchache baada ya kutoka mjini hapo.
Walishangaa sana kusikia habari hiyo, wakaanza kujiuliza mtoto wao alikuwa kapanda gari hilo kuelekea wapi! Walipojaribu kumuuliza mwalimu kuwa labda alikuwa na taarifa na hiyo safari naye aliruka kimanga na kudai hana ajualo.
Hapo ndiyo wazazi walizidi kuchekecha akili wakijiuliza kuwa mtoto wao alikuwa anasafiri kuenda wapi na ni kwa nini aondoke bila ya kuaga ama kutoa taarifa?
Hata hivyo hilo halikuwa la kujadili sana kwa wakati huo, kilichokuwa cha msingi kwa wakati huo ni kwenda hospitali kumuona mtoto wao, hata hayo maswali yao yote yangeweza kupata majibu hukohuko kwa kumuuliza mwenyewe.
“Au labda alikuaga wewe lakini unanificha tu?” Ilikuwa ni sauti ya babu yangu akimuuliza mkewe wakati gari yao inachoma mafuta kuelekea hospitali aliyokuwa kalazwa mama.   
“Aka! Mimi sijui chochote kuhusu safari hiyo, atakuwa kajiamulia mwenyewe.”
“Maana nyie wanawake wakati mwingine huwa mnakula njama na watoto wenu hasa hasa watoto wa kike.”
“Mimi siwezi nikafanya ujinga kama huo.”
            Mara baada ya maongezi hayo ukimwa ulitawala katika safari hiyo. Hawakuchukua muda wakawa wamefika kwenye hospitali ambayo majeruhi na maiti waliopatikana katika ajali ya asubuhi walikuwa wamehifadhiwa.
            Wakaanza kumtafuta mtoto wao kwenye wodi walizokuwa wameweka majeruhi. Kwa bahati nzuri hawakuhangaika sana wakawa wamemuona, ila alikuwa bado hajazinduka.
            Fahamu zilimrudia muda wa usiku, akashangaa kujiona yupo hospitali huku akiwa na majeraha mwili mzima. Hata hivyo tukio zima alilikumbuka mara baada ya kuvuta kumbukumbu. Ndipo akakumbuka kuwa  alikuwa akitoroka kwa kuogopa kugundulika nyumbani ya kuwa ni mjamzito.
            Akili yake ikamtuma kuwa huo ndiyo ulikuwa ni muda muafaka wa kuomba radhi kwa wazazi wake kwani hata zile hasira za baba yake zisingewaka sana juu yake kwa vile alikuwa anaumwa na yupo hospitali. Alijua fika mpaka kuja kupata nafuu baba yake atakuwa kashapunguza hasira kama siyo kuisha kabisa na hapo asingekipata kichapo cha paka mwizi.
Kesho yake asubuhi baba na mama yake walikuwa wameshafika hospitali hapo kumjulia hali. Kwa wakati huo hali yake ilikuwa inaendelea vizuri ingawaje alikuwa bado ana maumivu makali.
Ndipo alipopata fursa ya kuwaeleza wazazi wake kinaga ubaga juu ya tatizo lililokuwa likimsumbua kiasi kwamba mpaka akachukua uamuzi wa kutoroka nyumbani.
“Huyo bwege aliyekupa ujauzito huo ni nani na yuko wapi?” Lilikuwa ni swali la baba yake baada ya kusikia hivyo.
“Kashakimbia, hicho nacho ndicho kimechangia kunifanya nichukue uamuzi huo kwani ana wiki mbili sasa hayupo.” Alijibu mama yangu kwa shida.
“Jamani, mimi sioni sababu yoyote ya kuanza kuyajadili mambo haya huku hospitali, haya mambo ni ya kuyajadili tukiwa nyumbani.” Aliingilia kati bibi yangu.
            Hata hivyo mama alikuwa na hofu kwamba maelezo hayo akiyatoa wakiwa nyumbani yanaweza yakaupandisha ‘mzuka’ wa baba yake na kuanza kumshushia kichapo. Lakini alipiga moyo konde na kusema litakalokuwa na liwe. Kizuri zaidi alikuwa tayari kashatoa utangulizi wa jambo hivyo hasira za baba yake zisingekuwa nyingi sana.
            Baada ya wiki moja mama yangu aliruhusiwa kutoka hospitali, afya yake ilikuwa inaimarika vizuri ingawaje majeraha mengine yalikuwa hayajapona ikiwemo mkono wake ambao ulikuwa umevunjika hivyo alikuwa kawekewa ‘p.o.p’
            Siku hiyo hiyo alipofika nyumbani hakutaka kulaza damu, aliianzisha tena mada kwa kuwaomba msamaha wazazi wake kwa kile kilichokuwa kimejitokeza.
            Suala hilo liliongelewa na kufikia muafaka, akawa ameambiwa asiwe na wasiwasi kwani kuteleza si kuanguka.
“Usiwe na wasiwasi mwanangu mimi na mama yako tumeshakusamehe, ila ole wake huyo mpumbavu aliyejifanya rijali apatikane, hapo ndiyo atajua kuwa kumbe koti huwa halichomekewi, atajuta kuzaliwa.” Mzee wa kazi alimalizia kuongea kisha akaondoka zake.
            Mama aliendelea kuilea mimba yake akiwa nyumbani. Mpaka miezi tisa ilipoada ndipo alipojifungua mtoto wa kiume ambaye ndiyo alikuwa kifungua mimba wake, huyo hakuwa mwingine bali ni kaka James.
            Kuzaliwa kwa kaka James ndiyo kulikuwa hivyo. Wakati huo mimi nilikuwa bado sijafikiriwa hata kuiona hii dunia. Nilikuwa bado nipo mbinguni nikicheza na kufurahia tu na malaika.
ITAENDELEA......

Wednesday, October 23, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 34



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Gari lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani
    
                          **************************
SASA ENDELEA.......
Maisha ya jela ndiyo niliyoanza kuishi kwa wakati huo. Niligundua tofauti kubwa sana kati ya jela na mahabusu. Ukiwa mahabusu husumbuliwi kufanya kazi ama adhabu yoyote kwani unakuwa bado ni mtuhumiwa tu.
Lakini ukiwa jela unatakiwa kufanya kazi za hapa na pale zikiwa ni adhabu kwani tayari utakuwa umeshahukumiwa. Na ndiyo maana watu wengine husema jela kuna mateso.
Yote hayo ni tisa, kumi mkienda kulala, heheeeh! Kama utalemaa mithili ya kalio la kushoto basi unaweza ukawa mke wa wanaume wenzio. Huko ndiyo kuna watu waliopinda, watu wasiokuwa na dira na maisha.
Jela ni ubabe ubabe tu, unyama na mikwara ndiyo hutawala hasa kwa mtu mgeni gerezani humo. Hata hivyo kwa upande wangu hayo yote hayakutokea licha ya kuwa na muonekano wa upole.
Kilichonisaidia kutoionja adha ya ugeni wa jela ni kitu kimoja. Kuna jamaa mmoja nilimkuta humo gerezani ambaye tulikuwa tukifahamiana na kuheshimiana sana. Huyo mtu ndiyo alionekana kuwa msaada mkubwa sana kwangu kwani alikuwa kakaa humo kwa muda wa miaka miwili hivyo mikikimikiki ya huko alikuwa kashaizoiea.
Mbali na kuizoea mikiki mikiki ya humo; jamaa huyo alikuwa kashateuliwa kuwa mnyapara wa gereza. Mnyapara wa gerezani ni yule mfungwa anayewaongoza wafungwa wezake gerezani humo.
Jamaa huyo hakuwa mwingine bali ni Mack. Uhusiano wetu haukuanza siku hiyo ama siku za karibuni, ulianza miaka mingi iliyokuwa imepita. Tulikuwa tunafahamiana toka kitambo na tulikuwa tumeshafanya mambo mengi.
Baada ya kifo cha marehemu kaka James; mali zake zote nilizirithi mimi kwani ndiyo nilikuwa ndugu yake wa pekee. Ikumbukwe kuwa mimi na marehemu James tulizaliwa tumbo moja ila baba zetu ni tofauti.
Yeye ndiye alikuwa kifungua mimba katika tumbo la mama yetu. Mama yetu alipata ujauzito kwa bahati mbaya wakati anasoma elimu ya sekondari.
Baada ya kupewa ujauzito alilazimika kukatisha masomo ili aulee huo ujauzito hivyo akashindwa kuendelea na elimu na kujikuta akiishia kidato cha tatu.
Jamaa aliyekuwa amempa ujauzito alikimbia na kupotelea pasipojulikana kwa kuogopa kushtakiwa na wazazi wa mama yetu kwa kumrubuni na kumkatisha masomo mtoto wao.
Si wazazi peke yao waliokuwa wakila sahani moja na wanaume waliobainika kuwapa mimba watoto wao, hata serikali ilikuwa ipo mstari wa mbele kuhakikisha wanafikishwa mbele ya sheria.  
Tangu siku hiyo jamaa huyo alipotea kabisa na hakuonekana tena kama walivyopotea wadudu aina ya nzige. Nadhani waliozaliwa siku za nyuma kidogo wanakumbuka miaka ile ya uvamizi wa nzige katika mashamba ya wakulima.
Nzige ni wadudu hatari sana ambao hutembea katika kundi kubwa na wakivamia shambani mwako basi wanakula mimea yote iliyomo shambani humo. Usiombe shamba lako livamiwe na wadudu kama hao kwani wanakula hadi mashina ya mimea ya shamba wanalolivamia.
Sasa mwanaume aliyekuwa amempa ujauzito mama yetu na kumsababisha kukatisha masomo alipotea mithili ya wadudu hao.
Hakuonekana kabisa wala hazikusikika fununu zake hata kidogo. Kutokana na hiyo hali; mpaka wa leo haijulikani kama jamaa huyo bado yungali hai ama kashakumbwa na mauti.
Mama aliiingia katika wakati mgumu sana baada ya kubebeshwa huo ujauzito. Kilichokuwa kinamfanya apate tumbo joto ni jinsi baba yake alivyokuwa mkali na katili kupindukia, yaani marehemu babu.
Babu yangu huyo alikuwa ni mkali kama simba. Sijui kutokana na ujeshi wake aliokuwa nao, maana alikuwa mbogo kupita maelezo. Alikuwa hataki kabisa ‘Ujinga jazz bend’ katika familia yake.
Sasa ujauzito huo ulimfanya mama yangu azidi kuchanganyikiwa, kibaya zaidi hata aliyekuwa amempa huo ujauzito alikuwa kashakimbia na kutokusikika hata zile fununu zake.
Alichoamua ni kutoroka na kuenda asikokujua kwani aliona hata akienda kwa ndugu wengine baba yake angempata, na hapo ndiyo angelionja joto la jiwe.
Hakutaka kujiua wala kuitoa hiyo mimba kwani alikuwa akiijua vyema dhambi iliyopo kwa binadamu anayejiua ama anayeua. Hayo yote alikuwa ameyaweka akilini tangu utotoni alipokuwa akipewa mafundisho ya dini.
Mama yangu alilelewa katika maadili ya kidini sana japokuwa alikuja kuanguka dhambini na kurubuniwa na kamjamaa kalikokuja kumpa ujauzito.
Huku ujauzito aliokuwa nao ukiwa na miezi mitatu, mama aliamua kutorokea katika mji jirani ili kujiepusha na hasira za baba yake. Kwa mtazamo wake alihisi suluhu ya hiyo kashfa ni kulala mbele.
Alfajiri na mapema alitoka nyumbani kama anaenda shule akiwa na sare zake za shule huku nguo zingine akiwa ameziweka kwenye mfuko wake wa kubebea vitabu vya shule.
Kwa vile ilikuwa bado asubuhi sana, hakuna mtu yeyote  aliyemuona kwa pale nyumbani wakati anatoka. Alitembea mpaka kwenye stendi ya mabasi, akakata tiketi ya basi lililokuwa linaondoka muda si mrefu.
Wakati huo alikuwa tayari kashazivua sare za shule na kuvaa nguo zake za nyumbani alizokuwa ameziweka kwenye mfuko wa kubebea vitabu vyake vya shule.
Baada ya robo saa alikuwa tayari kajikausha kunako viti vya basi hilo huku likichanja mbuga kwa mwendo wa kasi.
Mambo yaligeuka kuwa si mambo mara baada ya basi hilo kuupa mgongo mji huo. Liligongana uso kwa uso na lori la mafuta na kusababisha ajari mbaya sana.
Basi hilo lilipiga mweleka na kubingirika mpaka mara tatu, likawa nyang’anyang’a kutokana na ajari hiyo.
Ilikuwa ni ajari mbaya sana na ya kutisha ambapo watu kumi na sita walipoteza maisha papo hapo, watu ishirini walikuwa ni mahututi na watu kumi na tano wakijeruhiwa ila siyo sana. Kati ya wale mahututi na mama yangu naye alikuwa ni mmoja wao.
Haukupita muda sana magari ya kubeba wangonjwa (ambulance) yakawa pale kubeba wahanga wa ajari hiyo pamoja na maiti na kuwapeleka katika hospitali ya jeshi iliyokuwa karibu kabisa na sehemu ilipokuwa imetokea ajari hiyo.
Mpaka anafikishwa hospitali mama yangu alikuwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa kaumia vibaya sana

                        ************************
ITAENDELEA.....!

Monday, October 21, 2013

MLANGONI MWA SABINA sehemu ya 33



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
          Baada ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.
SASA ENDELEA.......
Kwa namna moja au nyingine nilifurahi kusikia hivyo kwani nilikuwa na shauku kubwa ya kujua hatma ya hiyo kesi yangu. Japokuwa nilikuwa najua fika ya kwamba kuokoka kwangu ilikuwa ni bahati nasibu, kitendo cha kupelekwa mahakamani na kupandishwa kizimbani mara kwa mara kilikuwa kimeshanikifu.
Niliona ni heri hukumu yangu ikitoka, hata kama nitahukumiwa kunyongwa basi nitakaa gerezani bila bughudha siku zote za kungojea kunyongwa kwangu.
Niliteremka kizimbani na kuchukuliwa na askari magereza kwa ulinzi mkali mpaka kwenye karandinga lao kama ilivyo ada. Tulikaa kidogo kuwasubiri baadhi ya mahabusu ambao kesi zao zilikuwa zinaendelea kusikilizwa. Baada ya kukamilika wote, tuliondoka mahakamani na kuelekea magereza.

                        *****************************

Mwezi mmoja ulitimia tangu siku ambayo kesi yangu ilisikiliza. Hayawi hayawi hatimaye sasa yakawa, siku ya hukumu yangu iliwadia.
Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinidunda kasi kuliko kawaida. Pamoja na kwamba nilikuwa naiombea siku ya hukumu ifike, siku hiyo nilikuwa nimenyong’onyea na kuwa mpole kama shilingi mia.
Usiombe kuwekwa kizimbani kwa mara ya mwisho ukisubiri hukumu, tena hukumu yenyewe ya kesi ya mauaji! Hakika nilikuwa nipo maji siku hiyo.
Nilipandishwa kizimbani huku nikiwa nimenywea pasipo mfano. Yaani ilikuwa ni tofauti kabisa na siku zingine zote nilizofika mahakamani hapo.
Jaji alianza kusoma hukumu yangu kwa kutaja kosa lililokuwa linanikabili na kutangulia kusema kuwa adhabu ya kosa hilo ni kifo endapo mtuhumia atapatikana na hatia.
Niliposikia hivyo moyo wangu ulilipuka pu kana kwamba ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kusikia hiyo adhabu ya mtu mwenye hatia ya kuua.
Jaji huyo aliendelea kwa kusema kuwa hakuna shaka yoyote kwa ushahidi ambao ulitolewa ya kuwa nilimuua Kishoka Mpoto siku ya tukio hilo.
“Hata katika utetezi wake mshtakiwa kashindwa kutoa maelezo sawasawa ambayo yanaweza yakailinda hoja yake kuwa hajaua. Suala la kudai kuwa shahidi aliyetoa taarifa za tukio kituoni ni mchawi au ni jini haliwezi likaaminiwa na mahakama hata siku moja kwani hakuna uchawi juu ya sheria.” Aliendelea kutema maneno jaji Aneth Mwalukwa.
Aliendelea kusema kuwa ushahidi wa picha, alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichokuwa kimetumika kumuulia Kishoka vilikuwa ni vielelezo tosha kabisa kunitia hatiani.
“Japokuwa sababu au chanzo cha mtuhumiwa kumuua marehemu hakijafahamika mpaka sasa kutokana na mshtakiwa kuendelea kushikilia msimamo wa kwamba hajaua, bado haiondoi dhana ya mtuhumia kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.” Alizidi kusema jaji huyo.
“Kazi yangu ilikuwa ni kuchambua madai ya pande zote mbili, lakini upande wa utetezi umeonekana kuwa na hoja ambazo hazina mantiki kabisa, hoja za kusingizia ushirikia. Katika kusoma madai ya upande wa mshtakiwa sikuona shahidi yeyote ama ushahidi wowote ulioonyesha kuwa ni kweli mtuhumiwa hajaua zaidi ya maneno matupu ya kudai kuwa tukio liliambatana na ushirikina.” Aliunguruma mwanamama huyo.
Mpaka hapo matumaini yalikuwa yameshaniishia kabisa. Nilijua fika kuwa mwisho wa hukumu yangu ni adhabu ya kifo. Huku maelezo ya hakimu hayajafika mwisho nilianza kuhisi machozi yakinilengalenga huku pua zangu zikionekana kuloa.
Jaji aliendelea kusema kuwa jambo la shahidi aliyetoa taarifa polisi kutotokea kituoni haliwezi likaleta shaka yoyote juu yake kwani jambo muhimu ambalo ni kutoa taarifa alikuwa kashalifanya. Tena kwa kuongeza ushahidi aliamua kujitokeza mahakamani na kutoa ushahidi wa picha ambao ulionyesha hali halisi ya tukio lilivyokuwa.
“Kutofika kituoni huenda kulichangiwa na woga pamoja na kuchanganyikiwa kutokana na uzito wa tukio jenyewe ulivyokuwa.” Aliendelea kufafanua jaji huyo.
Ulikuwa ni uchambuzi ambao ulichukua karibu saa moja. Jaji Aneth Mwalukwa alihitimisha hukumu yake iliyokuwa na kurasa kadhaa kwa kueleza kuwa anakubaliana na upande wa mashtaka kuwa nilikuwa nimetenda kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya marehemu Kishoka Mpoto.
“Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu mtu anayepatikana na kosa hilo, adhabu yake ni kifo. Kwa hiyo natamka kwamba mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Brighton David kwa kosa la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudi.
Jaji alinyamaza kidogo kisha akanitazama na akuniambia,
“Mshtakiwa Brighton David nakuhukumu adhabu ya kifo, utanyongwa kwa kitanza mpaka ufe.”
            Jaji alipomaliza kusoma hukumu yangu aligonga nyundo mezani kisha akainuka na kuondoka.
            Kwa kweli sikuweza kujizuia. Nilijikuta nikiangua kilio cha haja huku simanzi na huzuni zikitawala kwa watu wengi waliokuwa wamefika mahakamani hapo, wale waliokuwa wananijua na hata wale ambao walikuwa hawanijui.
            Wakati jaji anaondoka mahakamani askari magereza walinishusha kizimbani na kuanza kunipeleka kwenye karandinga la magereza bila hata kunipa nafasi ya kuagana na baadhi ya watu niliokuwa najuana nao.
            Kijana niliyekuwa nimemuachia kuisimamia miradi yangu alikuja mbio akitaka kuongea nami kwa mara ya mwisho, lakini bila huruma askari alinisukuma na kunitaka niingie kwenye karandinga haraka.
            Gari lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani
    
                          **************************
HAYA SASA, HUKUMU IMESHATLEWA! BRIGHTON ATANYONGWA KWELI AU ITAKUWAJE? ENDELEA KUFUATILIA!