Monday, September 30, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 22



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Vijana hao niliwafananisha na mazuzu ambao mishipa ya fikra ilishakatika kichwani mwao. Rumande siyo sehemu ya kukimbilia kama una akili yako timamu.

                                    *************************
SASA ENDELEA.......            
Watu walikuwa wamefurika  kusikiliza kesi mbalimbali zilizokuwa zikiunguruma katika mahakama kuu ikiwemo kesi yangu. Kesi nyingi zilizokuwa zikitajwa siku hiyo zilikuwa ni za mauaji.
            Wakati huo nilikuwa nipo kwenye kizimba cha washtakiwa nikiapishwa. Mara baada ya kuapishwa, kesi ilisomwa.
            “Ni kweli au si kweli?” Lilikuwa ni swali la mwendesha mashitaka Charles Ngonyani ambaye alikuwa ni wakili wa serikari.
            Hata hivyo wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliniambia nikane, nami nikatikisa kichwa kukataa kisha nikasema,
“si kweli”
            Baada ya hapo kesi iliahirishwa tena kwa muda wa wiki moja ili upande wa mashtaka uanze kupeleka mashahidi wake.
            Nilirudishwa tena gerezani nikiwa bado mahabusu. Mpaka hapo nilikuwa nimeshaipata freshi ya kwenda na kurudi mahakamani, kesi yenyewe ilikuwa haijaanza hata kusomwa.
            Niliendelea kukaa rumande mpaka siku ya kesi yangu ikawadia tena. Siku ilipofika kama kawaida karandinga la magereza lilitusomba mpaka mahakamani mahabusu ambao kesi zetu zilikuwa zinasomwa siku hiyo.
            Shahidi aliyeanza kutoa ushahidi kutoka upande wa mashitaka alikuwa ni Sajenti Bakari Mlongo ambaye ndiye alikuwa amelibeba jukumu la kuipeleleza kesi yangu.
            Huku akiongozwa na wakili wa serikali, Sajenti Bakari Mlongo alieleza kuwa siku ya tukio akiwa kazini kwake kwenye kituo cha polisi cha kati alipigiwa simu kupitia simu ya kazini na mwanamke mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni ndugu yake na Kishoka.
“Baada ya mpigaji kujitambulisha hivyo aliwaambia nini?” Aliuliza wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani.
“Mtu huyo alieleza kuwa kuna mauaji ya kutisha yaliyokuwa yamefanyika kwenye nyumba ya bwana Brighton David.” Alisikika Sajenti Mlongo akijibu.
“Mtu huyo alieleza kuwa nani kauawa?”
“Ndiyo alieleza. Alisema kuwa aliyekuwa ameuawa ni ndugu yake aitwaye kishoka.”       
Sajenti Mlongo aliendelea kueleza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alitoka yeye na askari wengine wanne na kuelekea kunako eneo la tukio.
“Mlifika mpaka eneo la tukio?”
“Ndiyo tulifika.”
“Ikawaje?”
“Kwanza tulilikuta geti la ngome ya nyumba hiyo lipo wazi, tulipofika kwenye mlango wa kuingilia wa nyumba ya mtuhumiwa tuliuona uko wazi. Ndipo tulipoingia kwa tahadhari kubwa. Hata hivyo pale ukumbini hakukuwa na mtu zaidi ya runinga iliyokuwa imewashwa.”
“Baada ya kuona hapana mtu sebuleni mlichukua uamzi gani?”
“Tulijaribu kuangaza na kubaini kuwa mlango wa chumba kimojawapo kwenye hiyo nyumba  ulikuwa wazi na taa ilikuwa ikiwaka. Ndipo mimi na afande mmoja tuliingia kwenye chumba hicho.”
“Endelea kuieleza mahakama mlichokikuta baada ya kuingia kwenye chumba hicho!”
“Tulimkuta mtuhumiwa ambaye ni bwana Brighton akizunguka zunguka humo chumbani huku mwili wa Kishoka ukiwa kitandani huku kichwa kikiwa mbali na kiwiliwili chake. Vile vile kisu ambacho tulishuku kutumika katika kutekeleza mauaji hayo kilikuwa kikiambaa ambaa sakafuni.”
“Baada ya kuona hivyo mlichukua uamuzi gani?”
“Tulimuweka chini ya ulinzi mtuhumiwa, lakini kabla hatujamfunga pingu alianguka ghafla na kupoteza fahamu.” Aliongea Sajenti Mlongo.
“Huyo mtuhumiwa mliyemkamata siku hiyo ukimuona unaweza kumtambua?” Aliuliza wakili Charles Ngonyani.
“Ndiyo ninaweza.”
“Hebu ionyeshe mahakama tukufu mtu huyo kama yumo humu!”
“Yule pale kwenye kizimba.” Sajenti Mlongo aliongea huku akinisonta pale nilipokuwa.
            Wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia,
“Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.
KESI HII ITAISHAJE? USIKOSE SEHEMU YA 23!

Thursday, September 26, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu 22



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Baada ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.
SASA ENDELEA.......
            Tukiwa njiani moyo wangu ulizidi kuumia kwa kupotezewa muda kwa kesi ambayo sijashiriki wala kuifanya. Akili yangu yote ilikuwa kwenye hatima ya hiyo kesi. Mpaka tunafika kwenye ngome ya gereza nilikuwa nimezama kwenye mawazo mazito. Nilighutushwa na sauti ya mlango wa karandinga ulipokuwa ukifunguliwa ili tushuke. Tulishuka na kuswekwa kwenye gheto la watuhumiwa kuendelea na msoto.
            Wiki mbili zilikatika nikiwa rumande, niliziona ni nyingi sana. Hali yangu kiafya ilizidi kuwa mgogoro kila siku iliyoenda kwa Mungu. Kudhoofu huko hakukutokana na ugonjwa bali mawazo, aiseeeh! Acha kabisa kitu mawazo, tena mawazo ya kesi ya mauaji ambayo hukushiriki hata kuitenda. Kila wakati nilijikuta nikichoka kabisa.
            Wakili wangu alinitembelea tena siku moja kabla ya siku ya kwenda mahakamani. Tuliongea mawili matatu huku akinipa moyo kwa kuniambia nitashinda tu na haki itatendeka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
            “Halafu mbona umekonda sana?” Lilikuwa ni swali la Jonas Mlyanyama baada ya kuongea mambo yetu muhimu yaliyokuwa yanahusiana na hiyo kesi yangu.
“Mawazo kaka, unajua kesi hii inanipa wakati mgumu sana katika kichwa changu.” Nami nilimjibu.
“Acha kuwaza sana ndugu yangu, kwanza hii kesi mimi hainipi presha hata kidogo. Hapo tutashinda tu.” Alisikika wakili Jonas akiniambia.
            Maneno yake hayo niliyaona kama ya kunifariji tu ili niache kuwaza, lakini hatari iliyokuwa mbele yangu ilikuwa kubwa mno. Piga ua kifo cha kunyongwa kilikuwa kinaninyemelea. Suala la kuokoka lilikuwa adimu kama kaburi la baniani.
            “Najaribu kujikaza lakini najikuta nikiwaza tu, kila nikikaa mawazo yananijia, hata usingizi nashindwa kupata, chakula nacho hakipandi hata kama kwa kukilazimisha.”
“Usijali ndugu yangu, amini nakwambia Mungu yupo na atakusaidia.” Ilikuwa ni sentensi ya mwisho kutoka kinywani kwa wakili Jonas Mlyanyama.
            Bila ya muda kupotea tayari nilikuwa mbele ya askari aliyekuwa akilalama kuwa tumetumia muda mwingi kwa kupiga soga kama tumekutana sokoni.
            Alinipeleka moja kwa moja kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa lililokuwepo gerezani hapo. Nikawakuta mahabusu wenzangu ambao tulikuwa tumeshaanza kuzoeana.
Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale. Hata hivyo mimi mawazo yangu yote hayakuwa pale hata kidogo. Nilikuwa nikiwaza mambo lukuki kwa awamu, mara namuwaza Kishoka, mara nawaza kesi yangu itakavyokuwa.
Wakati mwingine taswira ya msichana aliyenisababishia matatizo hayo ilinijia kichwani mwangu; msichana ambaye mimi ndiyo nilikuwa nikiamini kwa asilimia mia tano kuwa ndiye alihusika na kifo cha Kishoka.
            Hali ya rumande ndugu yangu wee acha tu. Hata kama kungekuwa na masofa pamoja na runinga mimi nisingeweza kuyafurahia kwani uhuru hamna.
            Ilipofika mida ya jioni vijana wawili waliletwa kwenye ‘sello’ tuliyokuwemo. Mahabusu mmoja akaninong’oneza kuwa vijana hao walikuwa wameifanya rumande kuwa ni maskani yao.
            Kukatisha mwezi hawajaswekwa humo ilikuwa ni vigumu kwao. Kila waliporudi uraiani baada ya kumaliza kutumikia adhabu za vifungo walizokuwa wakipewa, vijana hao walifanya makosa tena na kurudishwa rumande.
            Niliwashangaa sana baada ya kuambiwa kuwa walikuwa na kasumba hiyo. Sehemu mbaya kama ile wao walikuwa wakiifurahia! Ama kweli kila shetani na mbuyu wake. Nilipojaribu kuuliza kipi hasa ambacho huwafanya waione rumande kama maskani niliambiwa kuwa ni ugumu wa maisha.
            Kumbe huo ndiyo ulikuwa ni mfumo wao wa maisha, si unajua tena huko kula ni bure na kulala ni bure! Kwao siku zilisonga kwa mtindo ule.
            Hata hivyo mimi niliona ni ujinga na umbumbumbu uliokuwa ukiwasumbua. Mbona kuna shughuli kibao huko uraiani ambazo wangefanya zingewapatia riziki ya halali.
            Vijana hao niliwafananisha na mazuzu ambao mishipa ya fikra ilishakatika kichwani mwao. Rumande siyo sehemu ya kukimbilia kama una akili yako timamu.

                                    *************************
ITAENDELEA........

Wednesday, September 25, 2013

MWACHENI MWANASHERIA AITWE MWANASHERIA!

Mwanasheria alifanya mapenzi na mwanamke kwenye gari, baada ya kufanya hicho kitendo mwanamke huyo alisahau chupi yake mle mle kwenye gari.
Mwanamke yule alisahau chupi yake humohumo kwenye gari.
Mke wa mwanasheria alipoingia kwenye gari akaiona chupi hiyo,
kwa vile alikuwa na wivu sana aliichukua na kuichanachana kwa hasira kisha akaanza kumfokea mume wake akimwambia kamsaliti.
Mwanasheria akasema,
"Umechana ushahidi katika kesi ya ubakaji na ningepata milioni nne kwa kesi hiyo"
Mke akaanza kujutia,
"Samahani sana mume wangu sikujua, ngoja basi niweke yangu inafanana na hii niliyoichana!"
Chezea mwanasheria weye!

Tuesday, September 24, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 21



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.
SASA ENDELEA.......
            Baada ya maongezi hayo yaliyochukua takribani saa moja wakili huyo aliondoka zake na kuniacha nikirudishwa rumande kusubiri siku yingine ya kusomwa kesi yangu.
            Niliendelea na msoto wa rumande. Kila siku mlo mmoja kwa siku huku chakula chenyewe kikiwa ni ugali wa dona na maharage yenye uozo. Maisha hayo nilikuwa sijawahi kuishi hivyo ilikuwa ni vigumu sana kuyazoea.
            Hata hivyo sikuwa na jinsi, nililazimika kujikaza kisabuni huku nikisubiri kudura za Wahidi ziniokoe katika hilo janga. Ilikuwa inauma sana hasa pale nilipofikiria jinsi uhusiano wangu ulivyokuwa na mpangaji wangu Kishoka ambaye nilikuwa natuhumiwa kumuua.
            Tuliisha kwa ushirikiano mkubwa kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu huku kila mmoja akiwa na meno thelathini na mbili; yaani akiwa mtu mzima.
            Sikuhusika na kifo chake, lakini nilikuwa nikishtumiwa ya kwamba nilimuua. Kwa mtindo huo kwa nini sasa roho isiniume? Ilikuwa ni zaidi ya uchungu.
            Siku ya kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena iliwadia. Asubuhi asubuhi mimi na mahabusu kadhaa tulisweka kwenye karandinga la askari magereza huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza.
            Mara baada ya kufikishwa mahakamani tulishushwa huku tukilindwa kwa silaha za moto, siraha nzito nzito za kivita. Mapaparazi nao walikuwepo kama kawaida yao, wakaanza kutusonga ili wapate picha za kwenda kutuuzisha sura runingani na magazetini.
            Licha ya kukaripiwa na askari magereza waliokuwa wametutanguliza, mapaparazi hao walizidi kukomaa ‘kutufotoa’ na kamera zao. Tukaingia mpaka mahakamani tayari kabisa kwa kuanza kusomewa mashtaka yetu kila mmoja kwa awamu.
            Mimi ndiyo nilianzia kupandishwa kwenye jukwaa la watuhumiwa kisha nikaapishwa kama zilivyo taratibu za mahakama kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
            Baada ya kuapishwa kizimbani kesi yangu ilitajwa. Hata hivyo jaji Aneth Mwalukwa aliiahirisha tena kesi ili kusubiri jalada la kesi kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka. Kesi yangu ilipelekwa mbele kwa muda wa majuma matatu.
Niliteremshwa kizimbani na kurudishwa kwenye sello ya hapo mahakamani kusubiri mahabusu wengine wamalize kusomewa mashtaka yao kisha turudishwe rumande.
            Baada ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.
ITAENDELEA......

HII NDIYO FACT YA LEO!

Hata kama uwe na heshima vipi huwezi kujiamkia,
"eti shikamoo mimi!"
Hahaaaaaaaaaaa! Utachekesha.

Monday, September 23, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 20



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Waliniamru nipande nami nikajitoma bila ya ubishi. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza. Gari lilitoka mbio utadhani lipo katika mashindano, tulitumia takribani dakika kumi kufika mahakamani.
SASA ENDELEA.......
            Tulipofika mahakamani tuliwakuta watu kibao, baadhi yao niliwatambua, walikuwa ni wakazi wa mtaani kwetu. Nilianza kuhisi kuwa taarifa za kesi yangu zilikuwa  zimetapakaa sana huko mtaani.
            Kamera za mapaparazi nazo zilizidi kunisonga wakati naingia mahakamani. Nilijaribu kujifunika usoni ili nisipigwe picha lakini haikusaidia chochote. Nilipelekwa mpaka sehemu ya kukaa watuhumiwa wakati wanasubiri kupandishwa kizimbani.
            Mara ilisikika sauti... ‘koooort!’, sauti hiyo iliashiria kufunguliwa kwa mahakama. Watu wote walisimama ili kutoa heshima katika mahakama kama ilivovyo ada, muda mfupi waliketi na kesi zikaanza kusikilizwa.
            Kesi yangu ndiyo ilikuwa ya kwanza kutajwa. Nilipandishwa kwenye kizimba kisha nikaulizwa dini yangu. Nilipotaja dini yangu nikapewa kitabu kitakatifu cha dini husika na kuanza kuapishwa.
            Baada ya kuapishwa nilisomewa shitaka langu na kuambiwa sitakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kuendesha kesi ya mauaji. Baada ya hapo nilitolewa kizimbani na kurudishwa rumande nikasubiri jalada la kesi yangu lipelekwe mahakama kuu. Lakini rumande niliyopelekwa kwa mara hii haikuwa ile ya kule kituoni bali ni rumande ya magereza.
            Nilikaa mahabusu katika rumande hiyo kwa siku kadhaa nikisubiri tarehe ya kutajwa kwa kesi yangu kwa mara ya pili ambayo ilitakiwa kuhamishiwa mahakama kuu, mahakama ambayo huwa na uwezo wa kuendesha kesi za mauaji.
            Kawaida ya sheria za nchi yetu ni kwamba, mshtakiwa yeyote wa kesi ya mauaji hutafutiwa wakili na serikali kama hana uwezo wa kumlipa wakili. Wakili huyo humsaidia kusimamia kesi yake mpaka mwisho.
            Hicho ndicho kilichotokea kwenye kesi yangu hiyo. Nilitafutiwa wakili ambaye alikuwa ni wakili kutoka kwenye taasisi moja inayosimamia haki za binadamu.
            Nikiwa nasota kwenye rumande ya magereza nilipokuwa nimepelekwa baada ya kutoka mahakamani, wakili alinifuata na kuanza kujadiliana nami jinsi ya kunisaidia katika kunitetea kwenye kesi iliyokuwa ikinikabili.
            “Hebu nieleze ukweli wako wote ili nijue ni jinsi gani nitakusaidia.” Alisikika wakili Jonas Mlyanyama kwa sauti iliyokuwa imejaa upole na yenye kubembeleza.
“Kusema kweli sikuhusika kabisa na kifo cha Kishoka.”
“Ilikuwaje, hebu niambia A mpaka Z bila kuficha kitu chochote.”
            Nilianza kumweleza tukio zima lilivyokuwa. Nikamweleza jinsi msichana wa kule ufukweni nilivyokutana naye na kuweka miadi ya kunitembelea kesho yake nyumbani kwangu.
            Sikuishia hapo, niliendelea kusimulia jinsi mauzauza yalivyoanza kujitokeza kwa mwanadada huyo pale alipokuja nyumbani na kukatalia getini baada ya kwenda kuambiwa na Kishoka apite ndani. Hata Kishoka alipokuja kuniambia kuwa mgeni huyo kakataa kuingia ndani bali ananitaka niende kulekule getini, nilienda lakini sikumkuta.
            Niliendelea kumhadithia kizaazaa hicho wakili Jonas Mlyanyama huku akiwa kanisikiliza kwa makini kabisa. Hatimaye nilimaliza maelezo yangu kwa kueleza jinsi nilivyoikuta maiti ya Kishoka ikiwa imelazwa juu ya kitanda changu.
            “Nimeambiwa kwamba alama za vidole vyako zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichotumika kumuua marehemu, ulikigusa kisu au ile maiti?”
“Hapana wakili sikugusa chochote hapo, na ndiyo maana nakuambia kwamba kesi hii ipo kimazingara. Hata mimi nashangaa kuonekana alama za vidole vyangu.”
            Wakili Jonas Mlyanyama alivuta pumzi kisha akazishusha. Wakati natoa maelezo wakili huyo alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo yangu kwenye kitabu alichokuwa amekuja nacho.
            Pamoja na kuwa ‘busy’ wakili huyo alionekana kuwa makini sana kunisikiliza kila nilichokuwa nakinena. Pia hakuacha kuhoji maswali pale ilipolazimu. Alikuwa na maswali mengi utadhani mgambo wa kata.
            Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.
JE, WAKILI JONAS MLYANYAMA ATAFANIKIWA KUMTETEA BRIGHTON KATIKA KESI YA MAUAJI YA KISHOKA? USIKOSE TOLEO LIJALO!